Iraq imekuwa timu ya mwisho kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika huko Marekani, Mexico na Canada baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na dhidi ya Bolivia katika Uwanja wa BBVA, Monterrey, Mexico.
Kufuzu huko kunaifanya Iraq imalize ukame wa miaka 40 wa kutoshiriki fainali hizo tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1986 ilipoishia hatua ya makundi.
Timu hiyo ambayo maandalizi yake kwa mechi hiyo ya mchujo wa mabara wa kuwania tiketi moja ya kushiriki Kombe la Dunia yaliathirika na vita inayoendelea Mashariki ya Kati baina ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, baada ya kufuzu, itakuwa katika kundi Ilenye timu za Ufaransa, Senegal na Norway.
Mabao kutoka kwa Ali Al-Hamadi na Aymen Hussein yameihakikishia Iraq ushindi huo ambao unawarudisha katika Kombe la Dunia baada ya muda mrefu kupita.
Baadhi ya wachezaji na sehemu ya benchi la ufundi la Iraq wakiwa katika picha ya kumbukumbu baada ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia kufuatia ushindi wa 2-1 walioupata dhidi ya Bolivia. Picha na Mtandao
Ushindi huo umeashiria mafanikio kwa kocha wa Iraq kutoka Australia, Graham Arnold, ambaye awali alikuwa ameomba mechi ya Jumanne iahirishwe kutokana na usumbufu uliosababishwa na mgogoro wa kikanda uliochochewa na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Wachezaji wengi wa kikosi cha Iraq waliwasili Mexico baada ya safari ngumu ya siku tatu kutoka Baghdad iliyoanza kwa kuvuka mpaka kwa njia ya nchi kavu kuelekea Jordan.
Bao pekee la Bolivia katika mchezo huo, limefungwa na Moises Paniagua katika dakika ya 38 akimalizia pasi ya Ramiro Vaca.
Iraq imeungana na timu nyingine tano za Taifa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kupitia mechi za mchujo.
Timu hizo za taifa ni DR Congo, Sweden, Uturuki, Bosnia & Herzegovina na Jamhuri ya Czech.