
Mwaka huu, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, hatua muhimu inayodhihirisha safari ndefu ya nusu karne kujenga na kusimamia ubora wa bidhaa na huduma nchini.
Katika kipindi hiki cha nusu karne, TBS imekuwa mhimili mkubwa wa kulinda afya ya walaji, kukuza ushindani wa bidhaa za ndani na kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu katika biashara ya kimataifa.
TBS ilianzishwa mwaka 1975 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi mwaka 1976 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za viwanda na biashara ili kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yak echini ya sheria ya viwango sura 130.
Hata hivyo, kadri uchumi wa Tanzania ulivyokua na mahitaji ya soko kubadilika, TBS ilipanua wigo wake na kuwa taasisi yenye ushawishi mkubwa katika sekta ya viwanda, biashara na afya ya jamii.
Ukuaji wa TBS ndani ya miaka 50
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi anasema katika kipindi cha miaka 50, TBS imekua kwa kasi kubwa na kupata mafanikio makubwa hususani katika utekelezaji wa majukumu yake. Mafanikio hayo yameendelea kutimiza azma ya Serikali katika sekta ya biashara hususani kuwezesha biashara ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wazalishaji kufikia masoko la kikanda na kimataifa.
Dkt. Katunzi anasema katika kipindi hicho pia shirika hilo limeshuhudia ukuaji mkubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ambapo wakati linaanzishwa lilikua na ofisi ndogo iliyokuwa imejengwa kwa mabati lakini hivi sasa lina jengo kubwa ambalo lina miundombinu za kisasa, uwepo wa maabara za kisasa pamoja na ujenzi wa maabara mpya katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Mwanza.
“Wakati shirika linaanzishwa kulikuwa na ofisi moja pekee iliyokuwepo Dar es Salaam lakini hivi sasa tuna ofisi kwenye mipaka, bandarini, viwanja vya ndege pamoja na ofisi za kanda tisa (Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa Mashariki, Kanda ya Ziwa Magharibi, Kanda ya Dar es Salaam na Kanda ya Kusini),” anasema Dk Katunzi.
Kuongeza idadi ya wafanyakazi ambao Dkt. Katunzi anasema wakati TBS inaanzishwa ilikuwa na wafanyakazi 30 pekee lakini hivi sasa ina wafanyakazi zaidi ya 800. Shirika pia limekuwa kimbilio la wafanyabiashara na wajasiriamali katika kuhakikisha bidhaa zao zinafika katika masoko ya kimataifa.
“Hivi sasa TBS imekuwa kimbilio la wafanyabiashara na wajasiriamali kuelekea masoko ya kimataifa. Hili ni jambo kubwa kwani wakati linaanzishwa watu walikuwa hawalielewi lakini hivi sasa limekuwa kimbilio lao,” anasema Dkt Katunzi.
Dkt. Katunzi anasema pia shirika hilo limeimarisha ukaguzi bidhaa kutoka nje Pre-Verification of Conformity (PVOC) ili kutatua changamoto ya bidhaa hafifu zinazoingia nchini.
“Mfumo huu unahakikisha bidhaa zote zinazoingizwa nchini zinakidhi viwango vilivyowekwa kabla hazijaingia sokoni. Hii imechangia kupunguza bidhaa hafifu sokoni,” anasema Dkt. Katunzi.
Uandaaji wa viwango
Moja ya majukumu makuu ya TBS ni kuandaa viwango vinavyotumika kudhibiti ubora wa bidhaa na huduma. Hadi sasa, maelfu ya viwango vimeandaliwa katika sekta mbalimbali kama vile chakula, ujenzi, kemikali, na bidhaa za viwandani.
“Shirika lina kamati za kitaalamu za uandaaji viwango 117 katika sekta za chakula, kemikali, uhandisi mitambo, uhandisi umeme, uhandisi ujenzi, nguo na ngozi, madini na mitambo ya uchimbaji madini, mazingira na sekta nyingine mtambuka,” anasema Dkt. Katunzi.
Dkt. Katunzi anasema katika mchakato wa kuandaa viwango, kamati hizo zinashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, bodi za wataalamu,
“Kwa kipindi cha miaka 50 shirika limefanikiwa kuandaa viwango zaidi ya 4000 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vinasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zinazopata masoko nje ya nchi,” anasema Dkt. Katunzi.
Umahiri na vifaa bora vya Maabara
Katika kuhakikisha ubora wa huduma zake, TBS imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maabara za kisasa. Maabara hizi zina vifaa vya hali ya juu vinavyowezesha kufanya vipimo sahihi na vya kuaminika.
“TBS ina jumla ya maabara 12 na zote zina ithibati za umahiri ambapo maabara hizi zimahakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa kimataifa. Hatua hii inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo yanaaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania,” anasema Dkt. Katunzi.
Anasema maabara zote za TBS zina mashine na vifaa vya kisasa hivyo kuwezesha kupata majibu kwa wakati na sahihi. Aidha katika kuunga mkono ajenda ya Serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, TBS ina maabara maalumu ya kupima viwavyo vya vifaa vinavyotumia nishati safi kutoka ndani na nje ya nchi (energy efficiency laboratory).
Uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA
Katika zama za kidijitali, TBS haijabaki nyuma. Shirika limewekeza katika mifumo ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano na wadau.
Dkt. Katunzi anasema wali shirika hilo lilikuwa linafanya shughuli zake kwenye makaratasi lakini hivi sasa kila huduma inapatikana katika mifumo jambo lililoongeza ufanisi wa utoaji huduma hivyo kulifanya shirika kuwa la kisasa na kuaminika zaidi.
“Kwa sasa shirika linatumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake mbalimbali kama vile leseni ya ubora, ukaguzi wa shehena zinazotoka nje na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi. Mifumo hiyo ni OAS na i-SQMT. Aidha shirika limeboresha huduma zake kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nchini kwa kuunganisha mfumo wake wa OAS na mfumo wa dirisha moja la huduma (TeSWS) ambapo mfanyabiashara anatuma maombi na kupata huduma za taasisi zote na kibali katika mfumo mmoja,” anasema Dkt. Katunzi.
Tuzo za umahiri na kutambulika kimataifa
Kwa juhudi zake katika kusimamia ubora, TBS inatambulika kimataifa na kushinda tuzo mbalimbali za umahiri. Mwaka 2023 TBS ilishinda tuzo ya mdhibiti bora barani Afrika na taasisi bora ya udhibiti Tanzania 2025, vilevile TBS imekuwa taasisi ya kwanza katika ukanda wa SADC kupata ithibati ya mifumo ya udhibiti ubora wa bidhaa katika wigo mpana ndani ya muda mfupi.
Vilevile TBS ina idhibati ya umahiri wa kimataifa katika mfumo wa Ukaguzi (ISO/IEC 17020. Mwaka 2025 TBS ilifanikiwa kupata ithibati ya umahiri wa mfumo wa usimamizi wa chakula katika kiwango cha kimataifa toleo jipya (ISO 22003: 2022). Pia shirika hilo kupitia wataalamu wake liliweza kutoa mshindi wa ISO Next Generation Award mwaka 2023.
Maadhimisho ya miaka 50
Dkt. Katunzi anasema kuwa katika kusherehekea miaka 50, TBS imeandaa matukio mbalimbali ambapo Mei 23, 2026 watafanya mbio za hisani (Viwango Marathon) zitakazofanyika katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, Juni 5, 2026 watafanya jukwaa la kibiashara (Viwango Business Forum) litakalofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Pia kutakuwa na zoezi la kurudisha kwa jamii (CSR) kabla ya hafla ya kilele cha maadhimisho hayo itakayofanyika Juni 19, 2026 jijini Dodoma.
Maadhisho ya miaka 50
Dk Katunzi anasema kuwa katika kusherehekea miaka 50, TBS imeandaa matukio mbalimbali ambapo Mei 23, 2026 watafanya mbio za hisani (Viwango Marathon) zitakazofanyika katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, Juni 5, 2026 watafanya jukwaa la kibiashara (Viwango Business Forum) litakalofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Pia kutakuwa na zoezi la kurudisha kwa jamii (CSR) kabla ya hafla ya kilele cha maadhimisho hayo itakayofanyika Juni 19, 2026 jijini Dodoma.