NI wanamuziki wachache wenye uthubutu wa kusema wimbo wake fulani ameandikiwa na mwenzake au walishirikiana kuandika, lakini wapo wanaoweka hilo wazi kama sehemu ya kuthamini mchango wa wenzao.

Kwenye Bongofleva kuna majina mengi makubwa na maarufu ambayo yameandikiwa nyimbo au kusaidiwa baadhi ya maeneo kiuandishi kama ifuatavyo.

1. Ben Pol; Wakati Lollipop (Goodluck Gozbert) akitengeneza muziki wa Bongofleva kama mtayarishaji, aliandika nyimbo nyingi za wasanii wa Bongofleva, miongoni mwa hizo ni Moyo Mashine (2016) wa Ben Pol, na ule wa Mo Music, Basi Nenda (2014).

2. Lulu Diva; Kwa mujibu wa mwimbaji huyu, alilazimika kumlipa Rich Mavoko fedha ili kumwandikia wimbo wake, Ona (2018) ambao walishirikiana, na baadaye ukawa wimbo wake wa kwanza kutazamwa mara milioni 1 YouTube.

3. Dogo Janja; Wimbo wa Dogo Janja, Banana (2018) umeandikwa na Marioo, na huu ulikuwa ni mradi uliosimamiwa na meneja wa Tip Top Connection, Babu Tale ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki. Pia Marioo amewaandika wasanii kama Christian Bella (Pambe), Gigy Money (Papa), Lyyn (Chafu), Shilole (Mchakamchaka), Mwasiti (Bado), Amber Lulu (Jini Kisirani), Ditto (Nabembea), Amber Lulu (Jini Kisirani) na kadhalika.

4. Hamisa Mobetto; Wimbo wa kwanza kuachia Hamisa, Madam Hero (2018) umeandikwa na Foby aliyefanya vizuri na wimbo wake, Niokoe (2018), pia ndiye amehusika kwenye kuandika na kutunga  melodi za wimbo wa Dayna Nyange, Komela (2016) akiwa na Billnass.

5. Diamond Platnumz; Mwanzilishi wa Billionea Kid, Rich Mavoko alimwandikia Diamond wimbo ‘Sijaona’ unaopatikana katika albamu yake ya tatu, A From Tandale (2018) iliyotoka chini Universal Music Group (UMG), kampuni ya kusambazaji muziki aliyojiunga nayo 2017.

6. Ruby; Uhusiano wake na Kusah ulikuja na vingi kwani Kusah ndiye ameandika wimbo wa Ruby, Ntade (2018) uliofanya vizuri. Pia wimbo uliomtoa Ruby kimuziki, Na Yule (2015) umeandikwa na Barnaba.

7. AY; Staa wa NLM, Rayvanny amechangia uandishi katika wimbo wa AY, Zigo Remix (2016), Ray alifanya hivyo katika ile vesi ya Diamond ambaye ameshirikishwa. Pia amefanya hivyo katika wimbo wa Diamond, Make Me Sing (2016) akiwa na AKA wa Afrika Kusini.

8. Vanessa Mdee; Kabla ya kuacha muziki, Vee alitoa wimbo uitwao Siri (2015) ambao uliandikwa na Barnaba ambaye ameshirikishwa pia. Hata wimbo, Chausiku (2018) walioshirikiana tena, Barnaba ndiye kaandika wote.

9. Alikiba; Wimbo wake, Dodo (2020) ameshirikiana kuuandika na Tommy Flavour, pia amefanya kitu kama hicho katika wimbo wake, Utu (2021) akiwa na Vanillah. Wote alioshirikiana nao katika uandishi amewahi kuwasaini katika lebo yake ya Kings Music.

10. Nandy; mwimbaji Jay Melody amemwandikia Nandy nyimbo nne ambazo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018), Hallelujah (2019), na Do Me (2020) ambao alishirikiana na mumewe Billnass. Pia Nandy, mwanzilishi wa The African Princess Label, ameandikiwa na wasanii wengine kama Aslay (Ninogeshe), Kusah (Nibakishie), Lody Music (Napona), Billnass (Dah!) na kadhalika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *