Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz, 36, kwa sasa anavuma na wimbo wake mpya, Happy (2026), ambao unaonyesha matunda ya ustahimilivu wake baada ya kuzikabili changamoto.

Kwa mashabiki wengi ni wimbo wa kawaida kama zilivyo nyimbo zake nyingine, ila kwa Diamond mwenyewe una maana kubwa akilinganisha na kule alipotoka hadi alipo kwa sasa.

Wimbo huo, ambao ni wa pili kuachia kwa mwaka huu baada ya awali kutoa Natulizana (2026), kwa sehemu umepata mapokezi mazuri hasa katika mitandao ya kijamii, ambapo wafuasi wake wamekuwa wakijivunia.

Kwenye wimbo huu (Happy), Diamond anaigeuza safari yake ya utafutaji kuwa sherehe baada ya kuzivuka siku za shida na kudharauliwa hadi sasa anapoishi maisha aliyokuwa akiyaota kwa miaka mingi.

Wimbo huu uliotayarishwa na S2kizzy, huku video yake ikiongozwa na Director Joma, una ucheshi na maneno ya kujiamini ambayo yamebeba hisia za ushindi. Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, anaonyesha kwamba wakati mwingine jibu sahihi kwa yaliyopita ni rahisi tu; nalo ni kusonga mbele, kusherehekea, na kuwa na furaha.

Safari ya Diamond haijawahi kuwa na changamoto tu wakati akitafuta kutoka kimuziki, bali hata baada ya kuwa maarufu amekumbana na vikwazo vingi kutoka kwa wadau na hata wasanii wenzake.

Katika wimbo wake ‘Baila’ kutoka katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018) chini ya Universal Music Group (UMG), Diamond alisema katika muziki anapigwa vita sana.

“Muziki vita, hawataki niendelee. Hivyo, ukipata nafasi, tafadhali niombe…,” anaimba Diamond katika wimbo huo aliomshirikisha Miri Ben-Ari, mshindi wa Grammy 2005.

Mstari huu ulikuja kipindi ambacho vituo vitatu vikubwa vya redio nchini pamoja na TV zake vilisitisha kabisa kucheza nyimbo za Diamond na hata kumzungumzia, hatua ambayo ilikuwa inatisha ukuaji wa kazi yake.

Hata hivyo, ukitazama kwa sasa, ni kama Diamond ameishinda vita hiyo kwa sababu naye tayari ana redio na TV yake, na wale waliozima kazi zake katika media zao sasa wamerejea kuzicheza na hata kumzungumzia.

Kwa hatua hiyo, sasa kwanini asiwe na furaha kama anavyoimba katika wimbo wake huo, Happy? Lazima afurahi kwa kupata suluhisho la kudumu la tatizo ambalo lilitaka kumpoteza kabisa kimuziki. Ukija katika lebo yake ya WCB Wasafi, hapa amewatoa wasanii wengi na wakawa na majina makubwa, na baadaye baadhi wakaamua kujitoa katika lebo hiyo na kwenda kuanzisha za kwao.

Katika mchakato huo wa kuhama, wapo waliodai Diamond hakuwatendea vizuri hata kidogo, lakini wao katika lebo zao mambo yamekuwa mabaya zaidi kiasi mashabiki wanaona Diamond alipakwa matope bila sababu.

Walioondoka WCB Wasafi na kumrushia Diamond maneno, nao lebo zao zimewashinda tena ndani ya muda mfupi, na malalamiko ya wasanii wao yanafanya Diamond aonekane mwema. Sasa kwanini asiwe na furaha?

Utakumbuka Diamond alitoka rasmi kimuziki kupitia wimbo wake, Kamwambie (2009), ambao ulibeba jina la albamu yake ya kwanza iliyoachiwa mwaka huo uliofuatia.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo kulipelekea kushinda tuzo ya kwanza ya muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010; kisha wakafuatia Linah (2011) na Ommy Dimpoz (2012), ambao wameshirikiana mara tatu.

Tangu 2013, aliwekeza upande wa digitali, na sasa hakuna msanii Afrika Mashariki anamgusa katika eneo hilo, huku akiwa na rekodi lukuki Afrika ambazo zinatokana na mauzo ya kazi zake mtandaoni, kitu ambacho wasanii wengi wanakitolea macho.

Ndiye msanii mwenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki, wa kwanza Afrika kufikisha views bilioni 2 YouTube, wa kwanza Afrika kushinda tuzo mbili za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs) kwa mpigo; sasa kwanini asiwe na furaha?

Kwa Tanzania, Diamond anatajwa kama mwanamuziki mwenye mafanikio zaidi kimuziki na kibiashara, ingawa hajawahi kuweka wazi utajiri wake ni kiasi gani, ila tunaweza kupata picha mara baada ya kuikata ripoti iliyodai utajiri wake ni Dola 5.1 milioni (takriban Sh12.7 bilioni).

Inaelezwa baada ya kuhitimu Sekondari 2006, Diamond alijikita rasmi katika muziki ili kujaribu kutimiza ndoto zake. Ili kuhakikisha anafikia ndoto yake, alifanya kazi mbalimbali, ikiwepo kuuza mitumba, kufanya kazi petrol station, na kupiga picha. Sasa kwanini asiwe na furaha kwa hapa alipo wakati huu?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *