Tumeyashuhudia ya mwezi huu hasa siku ya Machi 8, ambayo ilikuwa siku rasmi ya Wanawake Duniani inayoadhimisha kila mwaka.

Siku hii imepangwa kuwa rasmi, lakini kwa ujumla, mwezi huo wote wanawake kote duniani huendelea kuaadhimisha kwa kufanya mambo mbali mbali yanayowatambulisha na ni mwezi ambao hubeba ujumbe mzito wa kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo na kuhimiza usawa wa kijinsia.

Ndani ya mwezi huo, mjadala mpana huendelea katika majukwaa mbalimbali ukihusu uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Katika mijadala hiyo, wanawake hukumbushwa umuhimu wa kujitegemea kiuchumi, kujiamini, kushiriki katika nafasi za uamuzi na kujenga uthubutu wa kutumia fursa zinazojitokeza. Mafunzo kuhusu ujasiriamali, uwekezaji, matumizi sahihi ya fedha na uongozi hutolewa kwa wingi. Lakini changamoto kubwa imekuwa ni utekelezaji wa yale yote yanayojadiliwa kwa sabvabu ni shughuli inayofanyika kila mwaka.

Na kwa muda mrefu, imezoeleka kuona msisimko mkubwa wakati wa mwezi wa Machi, lakini baada ya hapo, kasi hiyo hupungua na hatimaye mambo kurejea katika hali ya kawaida. Binafsi nafikiri hali hii sasa inahitaji mabadiliko ya mtazamo.

Maarifa yanayopatikana katika kipindi hiki yanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko ya kweli, siyo kumbukumbu ya muda mfupi.

Na ni wakati sasa kwa wanawake kuchukua hatua madhubuti ya kuyageuza mafunzo wanayopata katika mwezi huo kuwa vitendo vinavyoleta matokeo.

Nathubutu kusema katika nyanja ya uchumi kwa mfano, wanawake wanapaswa kuthubutu kuanzisha na kuendeleza shughuli za kujipatia kipato. Iwe ni biashara ndogo au uwekezaji mkubwa, kinachohitajika ni uthubutu na nidhamu ya kusimamia rasilimali walizonazo.

Kwa mfano, badala ya kusubiri mtaji mkubwa, wanawake wanaweza kuanza na rasilimali walizonazo zitakazowasaidia kukua hatua kwa hatua. Pia kujiunga na vikundi vya kifedha kama vile vikoba au taasisi za kifedha ambako pia kunaweza kuwa njia mojawapo ya kuimarisha uwezo wao kiuchumi.

Katika eneo la uongozi, bado kuna pengo linalohitaji kujazwa. Ingawa juhudi zimefanyika kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uamuzi, idadi yao bado ni ndogo ikilinganishwa na wanaume. Hapa ndipo umuhimu wa kujiamini na kuondoa hofu unapojitokeza. Wanawake wanapaswa kuamini kuwa wana uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Ni muhimu pia kwa wanawake kujifunza sanaa ya kujitangaza na kusimamia taswira zao katika jamii. Katika dunia ya sasa, uwezo wa kujieleza, kuwasiliana na kujenga mtandao wa uhusiano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo binafsi na ya kijamii.

Aidha, mshikamano miongoni mwa wanawake unapaswa kupewa kipaumbele. Badala ya kushindana kwa njia zisizo na tija, wanawake wanapaswa kushirikiana, kusaidiana na kuinuana.

Nasema hivyo kwa sababu mafanikio ya mwanamke mmoja yanapaswa kuwa chachu ya mafanikio kwa wengine na isiwe chanzo cha migogoro au wivu.

Katika sekta ya elimu na maarifa, wanawake pia wanapaswa kuendelea kujifunza na kujiendeleza. Dunia ya leo inabadilika kwa kasi, na ujuzi wa zamani hauwezi kukidhi mahitaji ya sasa. Mafunzo ya teknolojia, biashara na hata stadi za maisha yanapaswa kupewa uzito unaostahili.

Hata hivyo, mafanikio haya yote hayawezi kupatikana bila nidhamu na uwajibikaji binafsi. Wanawake wanapaswa kujifunza kuweka malengo yanayotekelezeka na kuyafuatilia kwa umakini. Mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa juhudi na uvumilivu wa muda mrefu.

Ni muhimu pia kwa watu wanaowazunguka kuendelea kutoa ushirikiano kwao. Familia, taasisi na serikali zinalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa rafiki kwa wanawake kufikia malengo yao. Hata hivyo, msingi wa mafanikio hayo unabaki kuwa kwa wanawake wenyewe kuchukua hatua.

Zaidi ya yote, wanawake wanapaswa kutambua kuwa wao ni msingi wa maendeleo ya jamii. Wanapowezeshwa na kuchukua hatua, siyo wao pekee wanaonufaika, bali pia familia na vizazi vijavyo.

Kwa mtazamo huo, mwezi wa tatu haupaswi kuwa wa sherehe pekee, bali uwe mwanzo wa utekelezaji wa yale yote yaliyojadiliwa. Wanawake wanapaswa kuyachukua maarifa hayo na kuyageuza kuwa vitendo vinavyoleta mabadiliko ya kudumu.

Hatua ndogo ndogo zinazochukuliwa leo, ndizo zitakazojenga kesho bora. Wanawake wakiamua na kuchukua hatua, hakuna kitakachowazuia kufikia mafanikio wanayoyataka.

0713235309

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *