SIMBA inarudi uwanjani ikiwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye mchezo wa 16 baina ya timu hizo, lakini Wagosi wa Tanga, hesabu zinaonyesha, inaweza kuwa mechi ngumu kwao.

Simba itaingia kwenye mchezo huo na shauku kubwa ya kuendelea kuikimbiza Yanga, iliyo juu ya msimamo na ikiongoza ligi, ambapo kama ikishinda, itazidi kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya vinara hao.

Wekundu wa Msimbazi waliopo katika nafasi ya pili na pointi 31, wakiwa nyumbani wana moto mkubwa, kwani kwenye mechi zake tano zilizopita katika Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo wameshinda zote wakifunga mabao 14. Simba ikiwa Uwanja wa Isamuhyo msimu huu timu pekee iliyoambulia sare ni Mtibwa Sugar ya bao 1-1, lakini zingine zilifungwa kwa vipigo tofauti. Hata hivyo, Simba itawakumbuka Coastal Union, ikiwa ni moja ya timu zilizowatibulia kukosa ubingwa msimu uliopita, ilipotoka sare ya mabao 2-2 Oktoba 4, 2024.

SIMBA INAVIMBA HAPA

Wekundu hao wataingia wakiringia kiwango bora cha mastaa wake. Seleman Mwalimu anayeongoza kwa ufungaji ndani ya kikosi hicho, akifunga mabao matano, akifuatiwa na beki Rushine De Reuck mwenye mabao matatu, na viungo wengine mafundi, Lebase Gueye na Anicet Oura, ambao kila mmoja amefunga mabao mawili.

Hata hivyo, Simba itatakiwa kuwa makini na staa wao wa zamani, winga Shiza Kichuya, akiwa ndiye mchezaji mwenye takwimu bora ndani ya Coastal Union, akiwa na mabao manne.

Mbali na Kichuya, Coastal Union itamtegemea Maabad Maulid aliyefunga mabao mawili na asisti moja.

REKODI ZAIGOMEA COASTAL

Coastal Union itaingia kwenye mchezo huo ikitambua kwamba haijawahi kuifunga Simba, ambapo kwenye mechi 16 imefungwa 13, huku michezo mitatu ikimalizika kwa sare.

Wagosi hawako vizuri sana kwenye mechi za ugenini, ambapo ndani ya mechi tano za mwisho ikiwa ugenini, imepoteza mitatu, ikitoa sare moja, na kushinda mchezo mmoja pekee, ilipoichapa Prisons kwao 4-1.

Changamoto kubwa kwa Coastal Union, iliyopo nafasi ya 15 kwenye msimamo, ni kutofunga mabao, ambapo imefunga mabao 12 huku ikiruhusu 18 mpaka sasa kwenye ligi.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Coastal Union, Mohammed Muya, alisema kikosi chake kinakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya timu yenye wachezaji wazoefu, lakini wamejiandaa kutafuta matokeo mazuri.

“Tumekuwa na mapumziko mafupi na kurudi kazini. Kiasi kikubwa cha maandalizi yetu tumekuwa tukiboresha utengaji wa nafasi na kufunga; hali inaridhisha kidogo. Tunakwenda kukutana na timu nzuri yenye wachezaji wazoefu, lakini tutapambana,” alisema Muya. Kocha wa Simba, Steve Barker, akizungumzia mchezo huo alisema hakuna mchezo rahisi kwao, ambapo wanatambua kwamba Coastal Union imekuwa na matokeo ya kushtua na timu yake itataka kutengeneza ushindi mapema.

“Huwezi kuidharau timu yoyote kwenye ligi. Angalia mechi zetu zimekuwa ngumu sana, kwa hiyo tutaingia kwa kutafuta ushindi mapema. Tunaiheshimu Coastal Union; ni timu ambayo inaweza kufanya lolote likakushtua,” alisema Barker.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *