MUDA wowote kuanzia leo, vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), watakutana kwa ajili ya kupitia kesi inayomhusu mchezaji wa Yanga, Mohamed Damaro Camara dhidi ya Simba iliyofunguliwa kuhusiana na uhalali wa nyota huyo katika kikosi hicho cha Jangwani.

Katika kesi iliyopo TFF inaihusu Simba dhidi ya Damaro kuhusiana na uhalali wa mchezaji huyo kusajiliwa akiwa Mtanzania kwenye Ligi Kuu Bara ilihali mfumo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), anasomeka kuwa ni raia wa Guinea.

Madai ya Simba ni kwamba, kwenye mifumo ya TFF, Damaro anasomeka ni Mtanzania, lakini katika Fifa nyota huyo anatambulika kuwa raia wa Guinea akiwakilisha Shirikisho la Soka la Guinea (FEGUIFOOT), jambo ambalo ni kosa na kutofuatwa kwa taratibu.

Damaro akiwa na Singida Black Stars alisajiliwa kama raia wa Guinea kisha baadaye alibadili uraia na kupewa wa Tanzania na Yanga ilipomsajili wakati dirisha dogo la Januari 2026 ilimchukua kama raia wa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo kwa Yanga kumsajili akiwa Mtanzania na kumtumia bila kuomba kibali cha kubadili uraia wake kwa mujibu wa taratibu za Fifa, kupitia Kamati ya Hadhi ya Wachezaji (Players Status Committee – PSC), imeifanya Simba kufungua kesi TFF.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Evans Mgeusa alikiri kesi hiyo ipo mezani kwao na wiki hii wataanza kuipitia kisha watatoa uamuzi wa suala hilo.

“Kama ambavyo umesikia kuhusiana na madai yaliyowasilishwa na Simba ndivyo yalivyo. Kamati itakaa chini na pande zote mbili husika kwa maana ya Yanga, Simba na mchezaji mwenyewe kisha tuyapitie madai yaliyopo na tuamue,” alisema Evans.

Chanzo kutoka ndani ya TFF kimeliambia Mwanaspoti kwamba kwa sasa kumekuwa na vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili madai hayo ya Simba, ingawa mchakato uliopo ni wa ndani kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

“Vikao ni vya ndani, lakini suala lenyewe linatuumiza kichwa kwa kweli kwa sababu tunakosa hata muda wa kufanya pia mambo mengine. Yote kwa yote kwa sasa tunaendelea vizuri na naamini tutafikia muafaka wa jambo hilo,” kilisema chanzo hicho.

Damaro aliyejiunga na Singida Black Stars, Julai 27, 2024, akitokea Hafia ya kwao Guinea alibadilisha uraia na kupewa wa Tanzania sambamba na Emmanuel Keyekeh wa Ghana na Josephat Bada wa Ivory Coast.

Idara ya Uhamiaji ilithibitisha wachezaji hao watatu waliokuwa pamoja Singida Black Stars wamepewa uraia wa Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji Januari 23, 2025, ilisema Keyekeh, Bada na Camara waliomba na kupewa uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357.

“Wachezaji tajwa waliomba na kupewa uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357,”

“Kwa muktadha huo, Idara ya Uhamiaji inapenda kuutaarifu umma kuwa watajwa ni raia wa Tanzania kwa Tajnisi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa Januari 23, 2025 na msemaji mkuu wa Idara ya Uhamiaji, SSI. Paul J. Mselle.

MWANASHERIA, MDAU WATIA NENO

Akizungumzia suala hilo, mwanasheria Jacob Mashenene alisema mchezaji anaposajiliwa ni lazima aingizwe kwenye mifumo ya FIFA, hivyo ikiwa kutakuwa na changamoto yoyote wahusika wakuu ni TFF watakaopaswa kuwajibika kutokana na dosari iliyotokea.

“TFF wana mtu anayesimamia suala hilo vizuri, sasa kama kwa bahati mbaya alipitiwa na kushindwa kujiridhisha hadi kufikia hatua hiyo maana yake timu husika itakatwa pointi na mchezaji mwenyewe atapewa adhabu,” alisema Jacob.

Jacob alisema hata kama ikiwa mchezaji atakutwa na hatia timu anayocheza haiwezi kukatwa pointi kwa kila mechi, isipokuwa mamlaka husika itachagua alama za kukata kutokana na miongozo ya FIFA na TFF.

“Kama itaonekana kulikuwa na tatizo TFF itaamua pointi kadhaa za kuikata Yanga, lakini sio kwenye kila mechi aliyocheza. Inaweza kuwa pointi 10 kutegemeana na uamuzi utakaotolewa kwa sababu sio kosa la kujirudia rudia pia,” alisema Jacob.

Kwa upande wake nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema ikiwa kutaonekana na changamoto yoyote,  wahusika watapaswa kuwajibika kutokana na sheria na miongozo waliyojiwekea, ingawa mtazamo wake suala hilo lipo kishabiki zaidi.

“Wakati akiwa Singida Black Stars hatujasikia hizo kelele ila baada ya kuja Yanga tu tunaoana kila mtu anaongea jambo lake. Tusubiri uamuzi wa kamati ndipo nitakuwa na nafasi ya kuzungumzia ikiwa kutakuwa na hiyo shida,” alisema Chambua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *