Mbeya. Kupanda kwa bei ya mafuta hususani petroli, makali yameanza kung’ata jijini Mbeya baada ya usafiri wa daladala kuweka ‘mgomo’ kutoa huduma huku wananchi wakilia na nauli za bajaji zilizofikia Sh2,000 kutoka Sh800 za awali.
Mbali na wananchi, wapiga debe nao wamepaza kilio chao wakieleza kuwa hawaelewi hatima ya maisha yao kwa kuwa riziki zao zinategemea zaidi uwapo wa daladala wakiomba Serikali kukaa na wamiliki wa vyombo vya moto kulimaliza ili shughuli ziendelee.
Bei ya lita moja ya mafuta kwa Jiji la Mbeya Machi iliuzwa Sh2,996 na sasa imefika Sh3,952 kwa lita moja, hali ambayo imeonekana kutesa wananchi ambao leo baadhi yao wameamua kutembea kutokana na daladala kutotoa huduma na kiwango kipya cha nauli.
Kutokana na huduma ya usafiri wa daladala kukosekana, baadhi ya usafiri uliotumika ni gari dogo aina ya Noah, guta huku bajaji nazo zikitumika kutoa huduma kwa bei zaidi ya ilivyokuwa awali.
Wakizungumza leo Aprili 2,2026 baadhi ya madereva wa bajaji wamesema wamefikia hatua ya kupandisha bei ya nauli kutokana na bei ya mafuta kupanda tofauti na ilivyokuwa awali , huku madereva wa daladala wakiomba kupandisha hadi Sh1,500.
Baadhi ya wananchi wakipanda magari binafsi baada ya daladala kugoma kutoa huduma jijini Mbeya baada ya bei ya mafuta kupanda.
Kalulu Mashamba ambaye ni dereva daladala jijini humo amesema kufuatia bei ya mafuta kupanda, wao pia wanaomba nauli ipande hadi Sh 1,500 akieleza kuwa tofauti na hapo, biashara inawakata.
“Bei ya mafuta imepanda, sasa itakuaje tubaki na nauli ileile, kuna wanafunzi wanalipa Sh200 tutawaachaje? Hatujagoma ila tunaomba tupandishe pia nauli ifike angalau Sh 1,500” Amesema Mashamba.
Kwa upande wake dereva bajaji, Gervas Mwakyango amesema bei ya mafuta imepanda sana hivyo hata wao wapandishe nauli kufikia Sh2000 ili kuweka usawa kwa pande zote.
“Bora mafuta ingekuwa Sh3500 tungesema tupandishe nauli ifike Sh 1,000 kutoka Sh800, lakini kwa bei ilipofikia tumepandisha hadi Sh 2000 ili kupunguza makali” Amesema Mwakyango.
Naye mpiga debe wa daladala stendi ya Kabwe, Gervas Nsunga amesema kundi hilo limeathirika na mgomo huo kwa kuwa maisha yao yanategemea mzunguko wa watu na vyombo hivyo.
“Hatujajua tutakula wapi kwa kuwa maisha yetu kama njiwa, tunaomba serikali iingilie kati haraka tuweze kunusurika, daladala wamegoma wakitaka kupandisha nauli baada ya mafuta kupaa bei” Amesema Nsunga.
Muonekano wa stendi ya daladala Kabwe jijini Mbeya ikionesha kukosekana kwa daladala kufuatia mgomo baada ya kupanda kwa bei ya mafuta wakishinikiza kuoandisha nauli.
Mmoja wa wananchi jijini humo, Amad Noel amesema leo wamekutana na sintofahamu kutokana na kukutana na nauli za tofauti na walivyozoea akieleza kuwa hali hiyo imewashtua akieleza kuwa kwa sasa maisha ni magumu.
“Na hapa wanafunzi wamefunga kwa muda tunakutana na nauli kupanda, tunajiuliza hadi kumaliza likizo itakuaje, kutoka Uyole hadi hapa Kabwe tunatozwa Sh2000 usafiri wenyewe wa kuungaunga, serikali itusaidie maisha ni magumu” Amesema Noel.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema anaendelea na kikao cha wadau wote wa usafirishaji jijini humo, akifafanua kuwa baada ya mazungumzo ya pande zote Serikali itatoa msimamo na utaratibu kwa ujumla.
Muonekano wa stendi ya daladala Kabwe jijini Mbeya ikionesha kukosekana kwa daladala kufuatia mgomo baada ya kupanda kwa bei ya mafuta wakishinikiza kuoandisha nauli.
“Nipo kwenye kikao na wadau wote wa usafirishaji wakiwamo daladala, bajaji, gari kubwa na wengine wote, hivyo tukimaliza Serikali itatoa utaratibu kumaliza tatizo hili” amesema Itunda.