Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani asubuhi ya leo Alhamis tarehe pili ya mwezi Aprili, Katibu Mkuu uterres amesema mgogoro huo sasa umeingia mwezi wa pili, na kusisitiza kuwa kila siku inayopita inaongeza mateso ya kibinadamu, uharibifu, pamoja na mashambulizi yasiyochagua walengwa.

Amebainisha kuwa raia na miundombinu ya kiraia wanaendelea kulengwa, hali inayoongeza hatari si tu kwa eneo hilo bali pia kwa dunia nzima.

“Tuko ukingoni ‘kuingia’ vita vikubwa zaidi ambavyo vitaigharimu Mashariki ya Kati na kuwa na athari kubwa duniani,” amesema.

Picha ya pembe ya chini ya jengo la saruji la ghorofa nyingi lililoharibiwa sana huko Tehran, Iran. Mbele inaonyesha uharibifu mkubwa na saruji iliyo wazi, madirisha yaliyovunjika, na magofu yaliyotawanyika ardhini. Scaffolding inaonekana kwenye sakafu za juu.

© Mchangiaji

Jengo katika Mashariki ya Tehran likionesha uharibifu uliosababishwa na bomu.

Athari za kiuchumi na kijamii zaanza kuonekana duniani

Katibu Mkuu ameeleza kuwa mgogoro huo tayari una athari za kimataifa, hususan kutokana na kuzuiwa kwa uhuru wa usafiri wa majini katika njia muhimu kama Mlango-bahari wa Hormuz.

Ameonya kuwa hali hiyo inaathiri zaidi mataifa maskini na watu walio hatarini, huku ikichangia kupanda kwa bei za chakula na nishati katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Ufilipino, Sri Lanka na Msumbiji.

Wito wa kusitishwa kwa mapigano na kuimarishwa kwa diplomasia

Amesisitiza kuwa kuendelea kwa vita kutasababisha kuongezeka kwa maafa, akitoa wito wa kusitishwa kwa haraka kwa mapigano na kupewa nafasi juhudi za kidiplomasia zinazoendelea.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na kulinda uhuru wa mataifa na mipaka yao.

Katibu Mkuu pia ametangaza kumtuma mjumbe wake binafsi, Jean Arnault, kwenda katika eneo la mgogoro ili kusaidia juhudi za kutafuta suluhu ya amani.

“Ninamtuma Mjumbe wangu Maalum Jean Arnault. Lengo ni kuunga mkono jitihada za kikanda. Lazima tupate njia ya amani ya kutoka katika hali hii.” Amesema Guterres.

Katibu Mkuu António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu mgogoro wa Marekani-Israel-Iran, na bendera nyingi za kitaifa na nembo za baraza la usalama nyuma.

Picha ya UN/Mark Garten

Katibu Mkuu António Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuendelea kwa mgogoro wa Marekani-Israel-Iran na athari zake katika Mashariki ya Kati.

Ujumbe mahsusi kwa wahusika wa mgogoro

Katika hotuba yake, ametoa wito maalum kwa pande zinazohusika:

  • Ameitaka Marekani na Israel kusitisha vita mara moja
  • Ameitaka Iran kusitisha mashambulizi dhidi ya majirani zake

“Chaguo la amani bado lipo”

Akihitimisha, Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kuwa migogoro haiishi yenyewe bali humalizika pale viongozi wanapochagua mazungumzo badala ya uharibifu. “Chaguo hilo bado lipo  na lazima lifanywe sasa,” amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *