
SIMBA ilikuwa uwanjani jana dhidi ya Coastal Union, lakini kwenye mafaili ya mabosi wao kuna ripoti moja nzito kutoka kwa kocha Steve Barker iliyowasilishwa juu ya mastaa sita wanaotakiwa kikosini huku mmoja akiwa ameshapatikana.
Barker amewaambia mabosi kwamba kwa hesabu za msimu ujao anawahitaji wachezaji hao sita ili waje kuongeza nguvu kwenye kikosi chake kwa ajili ya kuendelea na maboresho.
Kwanza kocha huyo ametaka kutafutiwa mabeki wawili wa pembeni kuanzia kule kulia anakocheza mkongwe Shomari Kapombe na David Kameta ‘Duchu’ na kushoto anakomtumia Nickson Kibabage na Antony Mligo.
“Kule kulia kuna Kapombe ambaye anashauri kwa msimu ujao hataki awe anapewa mechi nyingi sana kutokana na namna alivyotumika sana ili kulinda kiwango chake lakini bado kocha ana wasiwasi kama Duchu kama anaweza kupandisha ubora wake,” amesema bosi mmoja ndabi ya Simba.
“Kushoto kwa sasa Nickson Kibabage kama ulivyoona anafanya vizuri sana tena tofauti na hata tulivyotarajia, lakini Mligo amepungua. Ukimkosa Kibabage sasa unaweza kupata shida. Ameshauri kama akipatikana beki mzuri zaidi au sawa na Kibabage itakuwa hatua nzuri.”
Eneo la kiungo limeguswa kwenye ripoti hiyo ya awali kocha huyo raia wa Afrika kusini akitaka asajiliwe kiungo mmoja mkabaji na mwingine mshambuliaji (namba nane) wenye ubora kushinda wale waliopo.
Kwenye hesabu hizo Barker ameonyesha hakubaliani sana na Alasane Kante na Naby Camara ambao kuna uwezekano mkubwa wakaachwa na Wekundi hao msimu ukimaliza.
Hata hivyo, tayari Simba imeshapata kiungo mkabaji ambapo Mwanaspoti linafahamu Kelvin Nashon msimu ujao atavaa jezi nyekundu na nyeupe akitokea Pamba Jiji baada ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo.
“Anataka pia kiungo mkabaji mmoja. Huyu tumeshampata tutawaambia baadaye na anatoka hapa hapa nchini kama akija pale kuungana na Kagoma (Yusuf) nadhani tutakuwa tumepata mtu sahihi kutokana na uwezo wake wa kukaba na umri wake.
“Kwa sasa tunatafuta namba nane hapa tunataka kutulia sana kupata mtu sahihi ambaye atakuja kutupa ubora mkubwa kwenye kikosi chetu,” amesema bosi huyo.
Kocha huyo anataka kusajiliwa washambuliaji wawili wenye ubora ambapo mmoja anatakiwa awe raia wa kigeni na mwingine mzawa.
“Huyu mshambuliaji anataka ambaye anaweza pia kucheza kama kiungo kuna mtu tunapambana naye ni sahihi sana lakini mshambuliaji mwingine awe mzawa kuna mmoja tunaendelea kupima kama atakuwa muafaka kwetu.
“Tunataka kumaliza usajili mapema ili kabla ya kumaliza msimu, hatutaki mambo ya presha za kuanza kugombea wachezaji ili tuwanufaishe madalali ndio maana tumeanza kazi mapema ili kila kitu kiwe kwenye afya ambayo tunataka.”