KIUNGO wa zamani wa Azam, Masoud Abdallah ‘Cabaye’ amesema kuwa kocha waliyenaye kwa sasa ni mtu sahihi sana, ila anahitaji muda ili kukijenga zaidi kikosi hicho.

Cabaye, ambaye amewahi kuzichezea timu mbalimbali kama KenGold, Azam FC, KMC na sasa akitumikia Tanzania Prisons.

Kocha Shadrack Nsajigwa alichukua kijiti baada ya klabu hiyo kuachana na Zedekiah Otieno kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya, huku akiiongoza timu hiyo katika mechi tatu za Ligi Kuu.

Tangu akabidhiwe kikosi hicho, bado hajapata nafuu ya matokeo, huku akipata suluhu dhidi ya Azam na kupoteza mbele ya Yanga 0-1 na Singida Black Stars 1-2.

Matokeo yaliyozidi kukiweka kikosi hicho kwenye hali mbaya, kikishika nafasi ya 15, kikiwa kimecheza mechi 17, kikishinda mitatu, sare nne na kupoteza 10, kikivuna jumla ya pointi 13.

Akizungumza na Mwanaspoti, Cabaye amesema kuwa Nsajigwa ni miongoni mwa walimu bora wazawa ambao yeye anawafahamu.

Amesema kuwa licha ya kwamba hajaanza vyema kazi yake kutokana na matokeo mabaya, lakini ni wazi kwamba anahitaji muda zaidi.

“Ni kweli tunaingia mzunguko wa pili, lakini bado mechi ni nyingi; kocha akipewa muda naamini ataleta mabadiliko sana, hasa kipindi tunachokianza.

“Mashabiki watulie; wachezaji tumefanya mazoezi mazuri. Natumaini tutarejea na nguvu mpya na kasi ya utofauti katika mzunguko unaofuata,” amesema Cabaye.

Baada ya mapumziko ya FIFA, Prisons itaanza na mechi ngumu ugenini dhidi ya Yanga, Jumamosi, Aprili 4, saa 12:30 jioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *