
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri na kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Mwaiyukule.
Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
Profesa Kabudi, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu, anachukua nafasi ya William Lukuvi, aliyefariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mshutuko wa moyo.
Mabadiliko hayo yametangazwa leo, Alhamisi, Aprili 2, 2026, na Bakari Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, akimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka.
Kuhusu Dk Mwaiyukule, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, atapangiwa kazi nyingine.
Aidha, Rais Samia amefanya mabadiliko ya naibu mawaziri. Reuben Kwagilwa, aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amehamishwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Nafasi ya Kwagilwa inachukuliwa na Dk Festo Dugange, aliyetoka kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Dk Dugange amewahi kuwa Naibu Waziri – Tamisemi.
Pia, Rais Samia amemteua Balozi Said Othman Yakub kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa. Awali, Yakub alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Samia amemteua Balozi Ali Mwadini kuwa Katibu wa Rais, akichukua nafasi ya Balozi Waziri Rajab, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Katika uteuzi huo, Rais Samia ameendelea kuzijaza nafasi zake 10 za ubunge, kwa kumteua Dk Eveline Munisi na Angela Kizigha, kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk Munisi, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia NCCR-Mageuzi.