Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge wameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza matumizi ili kukabailiana na nyakati ngumu za uchumi ambazo Taifa linaingia.

Kwa mujibu wa wabunge hao, eneo la kuanzia ni katika matumizi ya magari ya viongozi yakiwemo ya kwao, wakishauri Serikali iliangalie suala hilo ili kuokoa fedha zitakazowapelekea maendeleo wananchi sambamba na kudhibiti wizi.

Wametoa ushauri huo leo Alhamisi Aprili 2, 2026 wakati akichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilisha jana Jumatano Aprili Mosi na Dk Mwigulu Nchemba, aliyeliomba Bunge kuidhinisha Sh12.5 trilioni.

Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo amesema hatarajii kuona katika hali ngumu ya uchumi iliyopo, lakini watu wanaendesha mambo kama vile hakuna changamoto zozote hilo si jambo sahihi.

Katika maelezo yake, Shigongo amesema, “Hata katika familia ya kawaida, unapoingia katika nyakati ngumu kuna mambo ya kupunguza.

“Ombi langu mimi, natamani kuona tunaendesha maisha yetu kama Serikali katika kujibana kutokana na hali tulionayo,” ameeleza.

Ushauri wa Shigongo unakuja wakati huu ambao kuna kilio cha kupanda kwa gharama za mafuta yaliyopanda kwa takribani Sh1,000 kwa kila lita dizeli na petroli kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Kwa sasa wanunuaji wa mafuta ya rejareja yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam, wamelazimika kuongeza Sh956 kwa kila lita moja ya petroli baada ya bei kufikia Sh3,820 kutoka 2,864.

Wakati dizeli, wananua kwa Sh3,806 kwa lita moja kutoka Sh2,858 ikiwa ni ongezeko la Sh948. Hatua hiyo imetajwa kupandisha gharama za maisha hasa kwa watumiaji wa usafiri wa bajaji na bodaboda.

Ongezeko hilo limetokana na athari za mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati, yaliyosababisha Iran kufunga lango la Hormuzi linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta inayosafirishwa katika masoko mbalimbali duniani.

Hata hivyo, jana Dk Mwigulu aliwaambia Watanzania kuwa Serikali itaketi kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto ili wananchi kuendelea kupata nishati hiyo kwa bei nzuri.

Akiendelea kuchangia bajeti hiyo, Shigongo ameiomba Serikali kubana mianya yote inayosababisha kuvuja kwa mapato ya Taifa yanayopotelea mikononi mwa watu.

“TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) inafanya kazi kubwa sana kukusanya mapato, lakini fedha zetu zinapotea. Watu waaminifu wapo, lakini watu wabaya wapo pia,” amesema na kuongeza;

“Watu wanaoibia Taifa letu washughulikiwe kwa mujibu wa sheria, tuna sheria nzuri lakini hatuzimii kwa watu wanaotuibia. Hatuwezi kwenda mbele, kama wezi wanaendelea kuonekana katika Taifa letu, wanaoiba waende mahali wanapotakiwa kuwepo.”

“Nataka kuona Bunge hili chini ya Zungu (Mussa- Spika) wezi walishughulikiwa. Hatuwezi kuwa Taifa ambalo kila mwaka ikisomwa ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kuna mambo ya kutia aibu,” amesema.

Kauli hiyo Shigongo imekuja zikiwa zimepita siku nne kwa ofisi ya CAG kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Katika ripoti hiyo CAG amebaini uzembe na upotevu wa mabilioni ya fedha.

Akichangia mjadala huo, mbunge wa Nyasa, John Nchimbi amesema eneo la matumizi ya magari Serikali inatumia fedha nyingi, akisema ni wakati muafaka iangaliwe upya.

“Iangaliwe aina ya magari yanayotumika na kazi anazozifanya mtumishi. Utakuta mtumishi yeye ni mkurugenzi tena hapa hapa Dodoma na kazi zake hazimlazimu kutoka nje ya mkoa lakini anatumia gari la Sh480 milioni,”

“Kwa nini anatumia gari la gharama hiyo wakati haendi mbali? Serikali inatumia magari aina ya V8 zaidi ya 400, wakati kuna wengine hawakupaswa kuyatumia hayo,” amesema.

Nchimbi amefafanua kuwa hata hao wanaotumia V8 sasa hivi kuna tatizo la mafuta, lakini madereva wa magari wanayawasha kuanzia asubuhi hadi jioni yakisubiri viongozi.

“Unajiuliza hawa wanajua kama haya mafuta yananunuliwa kwa dola? Lakini ni gharama ya Serikali, mtu anangurumisha gari kuanzia asubuhi hadi mchana akimsubiri bosi wake ili lisipate joto,” amesema.

Mbunge huyo, amesema kama wabunge wanataka kudhibiti matumizi ya Serikali lazima yaanzie kwa viongozi wakiwemo wabunge hasa kwa magari wanayoyatumia mafuta.

Amesisitiza ni wakati muafaka kwa kuwekwa utaratibu wa udhibiti wa matumizi kuanzia mtu mmoja mmoja hadi serikalini ili kubana matumizi yatakayowezesha kuokoa fedha zitakazorudi kwa wananchi kuwapeleka maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *