Serikali yaokoa watoto 5,353 mitaaniSerikali yaokoa watoto 5,353 mitaani

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imea imefanikiwa kuwaokoa watoto 5,353 wanaoishi na kufanya kazi mitaani nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo inayoathiri ustawi wa watoto.

Akitoa taarifa kwa umma kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani yanayofanyika kila mwaka Aprili 12, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amesema kati ya watoto hao 5,007 wameunganishwa na familia zao huku wengine wakipatiwa malezi mbadala, mafunzo ya ufundi na huduma za kijamii.

Amesema juhudi hizo zinaenda sambamba na kampeni ya kitaifa iliyoanza Aprili 2025 kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto ikiwemo kuanzishwa kwa madawati 14 ya ustawi wa jamii katika vituo vya usafiri, ambavyo tayari vimehudumia zaidi ya watoto 2,600 na watu wazima zaidi ya 2,400.

Waziri Gwajima ameeleza kuwa sababu kuu zinazochangia watoto kuingia mitaani ni pamoja na umasikini wa kaya, migogoro ya kifamilia, ukatili dhidi ya watoto, vifo vya wazazi na athari za ukuaji wa miji akisisitiza umuhimu wa jamii kushughulikia chanzo cha matatizo hayo.SOMA: Serikali kuondoa watoto mitaani

Kwa mujibu wa wizara, Serikali pia imeendelea kutoa huduma za ulinzi na ustawi wa watoto kupitia makao maalum kama vile Kikombo na Kurasini p amoja na nyumba salama 18 zinazohudumia manusura wa ukatili, huku zaidi ya wazazi na walezi 469,000 wakipatiwa elimu ya malezi bora.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda haki za watoto na kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Malezi na Ulinzi wa Mtoto; Wajibu Wetu Sote”, huku akisisitiza kuwa hakuna sababu ya mtoto kuishi mtaani endapo jamii itashirikiana na mifumo iliyopo kutoa ulinzi na msaada kwa watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *