CHAMA cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTFC) kimeiomba Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kudhibiti matumizi ya tumbaku ili kupunguza madhara ya kiafya yanayosababishwa na bidhaa hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TTFC, Lutgard Kagaruki, wakati wa uzinduzi wa ripoti inayoangazia ushawishi wa makampuni ya tumbaku katika sera za afya nchini. Dk. Kagaruki amesema utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 2019 huku akibainisha kuwa Tanzania bado haifanyi vizuri katika kudhibiti matumizi ya tumbaku kimataifa.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), Peter Kisenge amesema magonjwa ya moyo ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani yakisababisha takriban vifo milioni 20 kila mwaka. Ameeleza kuwa matumizi ya tumbaku, uvutaji wa sigara, kiwango kikubwa cha sukari mwilini pamoja na shinikizo la damu ni baadhi ya sababu kuu za magonjwa hayo.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji Mwanaada Kilima, amesema mapato ya kodi yatokanayo na tumbaku ni takriban shilingi bilioni 200 kwa mwaka, huku gharama za matibabu kwa waathirika zikifikia zaidi ya shilingi bilioni 800. SOMA: Wakulima wa tumbaku kulipwa bil 13/- za mbolea ya ruzuku
Ripoti hiyo ya TTFC pia inaonesha kuwa Tanzania bado haijafanya vizuri katika kudhibiti matumizi ya tumbaku licha ya kuwa mwanachama wa World Health Organization (WHO) na kusaini mikataba ya kimataifa ya kudhibiti tumbaku.