Lindi. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa onyo kali kwa taasisi na mawakala wa meli nchini kujiepusha na vitendo vya kusafirisha wahamiaji haramu, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika.
Onyo hilo limetolewa leo, Aprili 2, 2026 na Ofisa Mfawidhi wa TASAC kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, Mhandisi Joseph Myaka, kutokana na tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika ukanda wa Kusini.
Amesema TASAC haitavumilia ukiukwaji wa sheria za usafirishaji wa baharini na imejipanga kuhakikisha nidhamu na usalama vinaimarishwa katika sekta hiyo.
Katika tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi, kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limewakamata wahamiaji haramu 70 waliokuwa wakisafirishwa kwa njia ya bahari.
Ofisa Mfawidhi wa TASAC kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, Mhandisi Joseph Myaka
Wahamiaji hao walikutwa ndani ya chombo kilichotambulika kwa jina la MV Sea Mfalme, kinachodaiwa kumilikiwa na mtu anatajwa kwa jina moja la Njomo. Taarifa za awali zimeeleza kuwa walikuwa wakitokea Mombasa, Kenya kuelekea Comoro, kinyume cha taratibu za uhamiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP John Imori, amesema tukio hilo lilitokea Machi 31, saa 10 usiku, katika Bandari ya Kilwa Masoko, wilayani Kilwa. Amebainisha kuwa kati ya wahamiaji hao, 10 ni wanawake na 60 ni wanaume.
Amesema mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wahusika.