Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali ya kibinadamu huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaendelea kuzorota kutokana na ongezeko la vurugu katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya UN tarehe 2 Aprili, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amenukuu mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa huduma za kibinadamu nchini humo yakisema kuwa mashambulizi kutoka makundi yaliyojihami yanaendelea kuathiri vibaya raia.
Mauaji Ituri
Katika jimbo la Ituri pekee, takribani watu 30 waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya Aprili Mosi, katika eneo la Bafwakoa, wilayani Mambasa, na kufanya idadi ya waliouawa kufikia zaidi ya 100 tangu Machi 11.
Wakati huo huo, zaidi ya watu 390 wameripotiwa kutekwa nyara katika kipindi hicho. “Vurugu hizo pia zimesababisha wimbi jipya la watu kuyahama makazi yao, na kuongeza idadi ya waliokimbia makazi kufikia zaidi ya 50,000 katika eneo hilo,” amesema Dujarric.
Huduma za afya zaporomoka huku mahitaji yakiongezeka
Mashirika ya kibinadamu yameripoti uporaji mkubwa wa vitu muhimu ikiwemo chakula, dawa na vifaa vya tiba kutoka vituo vya afya. Dujarric amesema, “tangu Machi 11, vituo tisa vya afya katika wilaya ya Mambasa vimesitisha huduma, hali inayowaathiri zaidi ya watu 55,000 waliokuwa tayari hawapati huduma za kutosha.”
Walinda amani wanaohudumu kwenye MONUSCO ikitekeleza jukumu lake la ulinzi wa raia huko jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC)
Hali Kivu Kusini
Katika jimbo la Kivu Kusini, takribani raia 20 wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa tangu Machi 23 katika mapigano yaliyotokea maeneo ya Uvira, Kalehe na Mwenga.
“Uharibifu wa makazi na mifugo umelazimisha familia nyingi kukimbia, huku upatikanaji wa chakula na huduma za afya ukiendelea kuwa mdogo,” ameeleza Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa.
Mapigano Masisi, Kivu Kaskazini
Katika jimbo la Kivu Kaskazini, mapigano yanayoendelea katika eneo la Masisi yamesababisha watu wapatao 6,000 kuyahama makazi yao kati ya Machi 28 na 29, na kuongeza idadi ya waliokimbia makazi kufikia zaidi ya 180,000.
UN yataka ulinzi kwa raia na msaada zaidi wa kifedha
Kwa mujibu wa Dujarric, licha ya hali ya usalama kuwa tete, mashirika ya misaada yanaendelea kutoa huduma pale inapowezekana.
Zaidi ya watu 30,000 walipokea msaada wa chakula katika mji wa Mweso kati ya Machi 16 na 27.
Hata hivyo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imezitaka pande zote zinazozozana kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kulinda raia na miundombinu yao, pamoja na kuruhusu upatikanaji wa misaada bila vikwazo.
Aidha, ombi la usaidizi wa binadamu kwa DRC linaendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.
“Kati ya dola bilioni 1.4 zinazohitajika, ni asilimia 30 tu—sawa na dola milioni 421—ndizo zimepatikana hadi sasa,” ametanabaisha Dujarric akiongeza kuwa, “Umoja wa Mataifa unasema kuna umuhimu wa haraka wa kuongeza ufadhili ili kukabiliana na mahitaji yanayozidi kuongezeka.”