Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge wameiomba Serikali kulipa kipaumbele suala la uboreshaji wa barabara hasa zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ili kuleta unafuu kwa wananchi.

Wabunge hao wametoa kilio hicho leo Alhamisi Aprili 2, 2026 wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilisha Jumatano Aprili mosi na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akiliomba Bunge kuidhinisha Sh12.5 trilioni.

Mbunge wa Ilemela (CCM), Kafiti Kafiti amesema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa vitovu vya kiuchumi, hivyo Serikali itupie jicho uboreshaji wa barabara zake ambazo baadhi si rafiki.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, barabara nyingi za Ilemela zimekuwa changamoto kubwa kutokana na kuharibiwa na mvua zilizonyesha kwa nyakati tofauti.

“Niwaombe sana Tarura kuangalia barabara za Ilemela ili kuhakikisha zinapitika kwa zimeharibika. Lakini barabara ya Uwanja wa Ndege hadi Kayenze ni kiungo muhimu, Serikali iiangalie kwa jicho la pili,” amesema.

Amesema endapo barabara hiyo itafunguka, itahamasisha maeneo makubwa ya kiuchumi kwa wavuvi waliopo mkoani humo wakiwemo wa Ilemela.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ameomba barabara ya kutoka Lushoto-Lukozi hadi Mtaya na nyingine kutoka Malindi hadi Mtaya, ziingie katika usanifu kwa ajili ya matengenezo ili kulifungua jimbo hilo.

“Lushoto tunaposema barabara, ndio kipaumbele chetu namba moja hadi namba tatu, kwa sababu tunapata bidhaa kutoka maeneo mengine kwa gharama kubwa kutokana na barabara zilizopo kutokuwa na uwezo wa magari makubwa,” amesema Shangazi.

Kutokana na hilo, Shangazi ameiomba Serikali kuboresha miundombinu hiyo ili kuwezesha magari makubwa ikiwemo malori na mabasi kupanda katika milima ya usambaa.

Naye, mbunge wa viti maalumu (CCM), Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge aliungana wabunge wengine kuiomba Serikali kuipata Tarura fedha ili kukarabati na kuzitengeneza barabara nyingi zilizoharibika.

Mbunge wa Chemba (CCM), Kunti Majala amesema Tarura wana barabara nyingi za udongo, hivyo inatakiwa kuondokana na barabara hizo na kuhamia kiwango cha changarawe ili kuboresha miundimbinu hiyo.

“Mvua kama hizi zinaponyesha barabara zetu zote zinaharibika kwa wakati mmoja. Bado tuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara inayosababisha watumishi wanaoletwa Chemba kushindwa kukaa kutokana na gharama ya usafiri kuwa kubwa,”   amesema.

Majala ameomba katika bajeti ya 2026/27 majimbo ya vijijini yamepewe kipaumbele kwa kutengenezewa barabara zitakazowezesha watumishi wa umma kupata ahueni ya kuwahudumia Watanzania.

Majala amesema amekuwa akifuatilia ziara za waziri mkuu na jambo kubwa ambao limekuwa likijitokeza katika mikutano yake ni migogoro ya ardhi.

“Kila mkoa na wilaya aliyokwenda Waziri Mkuu, amekutana na changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo imekuwa donda sugu katika Taifa letu,” ameeleza Majala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *