
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo, kimelaani uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wa kusitisha leseni ya kituo cha televisheni ya mtandaoni cha Jambo TV, kikieleza hatua hiyo ni tishio kwa uhuru wa habari nchini.
TCRA ilitangaza kusitisha leseni ya uendeshaji wa maudhui ya Jambo TV jana Aprili 2, 2026, maudhui ambayo hawakuwa na uhakika nayo na yasiyo na uthibitisho.
Ilisema maudhui hayo pia yaliupotosha umma kuhusu hali ya matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na matokeo yanayotarajiwa kutoka kwa Tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kinyume na kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025.
Aidha, mamlaka hiyo imesema katika kipindi kifupi cha takribani miezi sita sasa, yaani tangu mwezi Septemba, 2025, Jambo Online TV imekuwa na mashauri manne (4) mfululizo ya ukiukaji wa sheria, kanuni, masharti ya utangazaji wa habari.
Kwa sababu hiyo, mamlaka hiyo imesema imeisitishia Jambo TV leseni yake kwa siku 90 yaani miezi mitatu.
Kufuatia uamuzi huo, taarifa ya ACT Wazalendo iliyotolewa leo, Ijumaa Aprili 3, 2026 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo imelaani ikisema ni ukiukaji wa uhuru wa maoni.
Imesema ni mwendelezo wa kile ilichokiita ukandamizaji wa uhuru wa habari unaofanywa na Serikali, ikilenga kuzuia taarifa zinazoweza kuibua mjadala kuhusu matukio nyeti nchini.
“Tunaona hatua hii si tu inaathiri uhuru wa vyombo vya habari, bali pia inazua maswali kuhusu dhamira ya Serikali katika kulinda haki za msingi zilizowekwa kikatiba,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, chama hicho kimesisitiza masuala ya mauaji yanayodaiwa kutokea wakati wa uchaguzi mkuu si ya kufichwa, kwani yanaathiri moja kwa moja wananchi, huku baadhi ya familia zikiendelea kubeba maumivu ya kupoteza wapendwa wao.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimeonya kuwa kufungiwa kwa vyombo vya habari kuna athari pana, ikiwemo kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa na kutoa maoni, pia kunaathiri ajira za vijana wanaotegemea sekta ya habari kujipatia kipato.
ACT Wazalendo kimetoa wito kwa Serikali kubadili mwenendo huo na kuhakikisha Jambo TV inarejeshewa leseni yake bila masharti, huku kikihimiza Watanzania kusimama kwa pamoja kulinda misingi ya haki na uhuru wa kujieleza.
“Tutaendelea kupigania uhuru wa habari na haki za raia hadi pale zitakapoheshimiwa kikamilifu,” imeeleza taarifa hiyo.