
Italia imewaweka kipaumbele makocha wanne ambao mmojawapo ataziba nafasi ya Gennaro Gattuso anayejiandaa kujiuzulu Ukocha Mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kushindwa kuiongoza kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Makocha hao ni Roberto Mancini, Antonio Conte, Jose Mourinho na Massimiliano Alegri.
Italia ‘Azzuri’ ilipokea kichapo cha mikwaju ya penalty 4-1 kutoka kwa Bosnia na Herzegovina Jumanne iliyopita, jambo lililoifanya ishindwe kufuzu Kombe la Dunia, mashindano yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Kushindwa huko kwa Italia kufuzu Kombe la Dunia kumeibua presha kubwa kwa Gattuso na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Italia (FIGC) wanaotakiwa kujiweka kando.
Presha hiyo imesababisha Rais wa FIGC, Gabriele Gravina pamoja na kipa wa zamani wa Italia, Gianluigi Buffon ambaye amekuwa ndio mkuu wa msafara wa Italia wote kujiuzulu.
Na inaripotiwa sasa kwamba Gattuso yuko mbioni kujiuzulu kama ishara ya kuwajibika kwa matokeo hayo yasiyovutia ya kutofuzu Kombe la Dunia.
Kumekuwa na mapendekezo pia kwa Gattuso kwamba abakie hadi Juni ambapo Italia itacheza mechi mbili za kirafiki lakini kiungo huyo wa zamani wa Azzuri inaripotiwa hayuko tayari kufanya hivyo.
Na ripoti kutoka Italia zinawataja Conte, Mancini, Mourinho na Alegri kama watu wanaofikiriwa na FIGC katika mchakato wa kumrithi Gattuso.
Mancini anayeinoa Al Sadd ya Qatar hivi sasa, ndiye aliiongoza Italia kushinda taji la mashibdano ya Euro 2020 lakini baadaye akajiuzulu baada ya kushindwa kuiongoza Italia kutofuzu Kombe la Dunia 2022.
Meneja wa Napoli, Antonio Conte naye anafikiriwa katika mchakato huo akikumbukwa kwa namna alivyoiongoza Italia hapo nyuma huku ikiwa na kikosi dhaifu na kuifikisha hatua ya robo fainali katika Euro 2016.
Pia Alegri na Mourinho wapo katika orodha hiyo ya wanaotazamwa kama watu sahihi wenye sifa za kuiongoza Italia baada ya Gattuso.