Hakika Sharia tukufu ya Kiislamu ni kamili na yenye kujumuisha kila kitu, inayofaa kwa kila zama na kila mahali.

Miongoni mwa ukamilifu wake ni kwamba imejibu kila suala na kutoa hukumu ya Kisharia kwa kila tukio. Hili linafanyika kupitia vyanzo vyake vya sharia (mihimili): Qur’ani, Sunna, Ijmaa (Makubaliano ya pamoja ya wanazuoni). Qiyas (ulinganifu wa Kisharia).

Hivyo, Uislamu haukuacha jambo lolote dogo au kubwa bila kulibainisha, ama kwa ufafanuzi wa kina au kwa ujumla.

Katika safu hii, nitazungumzia kuhusu hukumu zinazomhusu mwanamke mjamzito aliyepata ujauzito kwa njia ya uzinzi. 

Hili linaonyesha wazi kuwa  Uislamu umeipa familia umuhimu mkubwa sana, ukasisitiza iwe imara na ishikamane na dini pamoja na maadili mema.

 Hii ni kwa sababu familia ndizo msingi wa jamii; ikiwa familia ni imara na safi, basi jamii pia hunufaika na kuwa bora. Lakini ikiwa familia ni dhaifu na imejaa maovu, matokeo yake huwa ni jamii iliyojaa upotovu na maadili mabaya.

Miongoni mwa mambo ambayo Uislamu umezingatia ni kulinda nasaba ya mtoto aliye tumboni. Kwa sababu hiyo, umeharamisha ndoa ya mwanamke mjamzito mpaka ajifungue. Ni lazima kufahamu kuwa Uislamu umeharamisha baadhi ya matendo kwa sababu ya madhara yake katika jamii.

Miongoni mwa hayo ni uzinzi na mambo yanayosababisha uzinzi. Mfano kuchanganyika kiholela kati ya wanaume na wanawake, kukaa faragha kati ya mwanaume na mwanamke wasiokuwa maharimu, kutoka bila hijabu na mengineyo. Haya yote yameharamishwa kwa sababu ni njia zinazopelekea maovu makubwa.

Ibn al-Qayyim (Allah Amrehemu) anasema: Kwa kuwa malengo hayawezi kufikiwa isipokuwa kupitia njia na sababu zinazopelekea kuyafikia, basi njia hizo hufuata hukumu ya malengo hayo na huzingatiwa kwa msingi wake.

Hivyo, njia zinazosababisha mambo ya haramu na maasi huchukiwa na huzuiwa kulingana na jinsi zinavyopelekea kwenye malengo hayo na uhusiano wake nayo. Vilevile, njia zinazosababisha utiifu na ibada hupendwa na kuruhusiwa kulingana na jinsi zinavyopelekea kwenye malengo hayo.

Suala linalojadiliwa hapa ni, je, Sharia ya Kiislamu inaruhsu kumuoa mwanamke mjamzito aliyepata ujauzito kwa uzinzi? Jibu lake, ikiwa mwanamke mzinzi ni mjamzito, wanazuoni wamehitilafiana kuhusu sharia ya ndoa yake.

Kauli ya Kwanza: Ndoa hiyo ni batili na haramu. Hivyo, hawezi kuolewa mpaka ajifungue. Na ikiwa si mjamzito, basi atalazimika kukaa eda pia. Huu ni mtazamo wa madhehebu ya Malik, Hanbali.

Baadhi ya wanazuoni wanasema anatakiwa kusubiri (istibra’) kwa kuingia hedhi tatu au miezi mitatu, na wengine wanasema hedhi moja inatosha, kwa sababu si mke halali.

Hoja yao ni kauli yake Allah Mtukufu: “Na wanawake wajawazito muda wao ni mpaka wajifungue mimba zao.  (65:4)” Aya hii inaonyesha kuwa mwanamke mjamzito anatakiwa kukamilisha eda yake kwa kujifungua, iwe ujauzito umetokana na ndoa halali au uzinzi.

Hivyo, aya ni ya jumla na inawahusu wanawake wote wajawazito bila kutofautisha chanzo cha ujauzito. Ushahidi wa Qiyas (ulinganifu wa Kisharia), kama ambavyo haifai kufunga ndoa na mwanamke mjamzito kwa mimba isiyo ya uzinzi, basi vivyo hivyo haifai kwa mwanamke mjamzito kwa mimba ya uzinzi.

Kauli ya pili inasema kuwa inaruhusiwa kufunga ndoa na mwanamke mzinzi, awe mjamzito au si mjamzito, hata kama mimba si ya huyo anayemuoa, na haishurutishwi kusubiri kumalizika kwa eda. Kwa mujibu wa kauli hii, inaruhusiwa kumuoa hata kabla hajajifungua.  Huu ni mtazamo wa Imamu Shafi na Ibn Hazm. Hoja yao ni auli ya Allah Mtukufu: “ “Mmeharamishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na mama wadogo zenu, na binti za ndugu zenu wa kiume na wa kike,…..”  (4:23)

Maana ya aya hii imewataja wanawake waliokatazwa kuolewa. Kisha baada ya hapo Allah amesema: “Mmehalalishiwa walioko nje ya hao.” Kwa maana, inaruhusiwa kuoa wanawake wengine wasiokuwa katika orodha hiyo. Kwa hiyo, mwanamke mzinzi mjamzito hayumo katika waliotajwa kuwa ni haramu, hivyo inaruhusiwa kumuoa.

Kauli ya tatu inasema kuwa inaruhusiwa kufunga ndoa na mwanamke mzinzi mjamzito, awe amepewa mimba na huyo anayemuoa au mtu mwingine, na hana eda kwa mujibu wa madhehebu ya Hanafi.

Ama ikiwa mwanamke tayari ni mjamzito, basi ndoa inasihi kufungwa, lakini hairuhusiwi kumuingilia mpaka ajifungue. Hoja yao ni kauli ya Allah Mtukufu:

“Mmehalalishiwa walioko nje ya hao.” Maana ya aya ni  kwamba mwanamke mzinzi hakutajwa miongoni mwa waliokatazwa, hivyo inaruhusiwa kumuoa na ndoa yake inakuwa sahihi.

Katazo la kumuingilia mwanamke mjamzito ni kwa mujibu wa Kauli ya Mtume wa Allah: “Mwenye kuamwamini  Allah na siku ya mwisho basi  asichanganye maji ya mwanaume na mimba ya mwingine” (Abu Daud)

Kauli sahihi kwa mtazamo wangu mwandishi, ninaona kuwa ndoa ya mwanamke mzinzi mjamzito ni haramu mpaka ajifungue, kwa sababu Uislamu unalinda familia na nasaba. Hivyo, ni lazima kusubiri mpaka ajifungue, kisha baada ya hapo ndoa inaruhusiwa.

0712 690811

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *