MSHAMBULIAJI wa Simba, Seleman Mwalimu wikiendi hii huko Chamazi, atakuwa na kibarua cha kuvunja rekodi yake ya mabao aliyoweka Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 akiwa na Fountain Gate kabla ya kutua Wydad Casablanca ya Morocco.

Bao ambalo alifunga Mwalimu katika mchezo uliopita wa Ligi wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga lilimfaya kufikia idadi ya mabao sita ambayo alifunga msimu huo.

Wakati Simba ikihitaji kulipa kisasi dhidi ya Azam kufuatia kupoteza mechi ya mzunguko wa kwanza kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Mwalimu atakuwa akisaka kuvunja rekodi hiyo.

Kwa sasa Mwalimu ndiye mshambuliaji kinara kwa wekundu hao wa Msimbazi akifunga mabao mawili katika mechi mbili za mwisho, kabla ya kuitungua Coastal alifunga pia dhidi ya TRA wakati Simba ikienda katika mapumziko ya michezo ya kimataifa na ushindi wa mabao 3-0.

Katika mechi nne za mwisho kucheza, Mwalimu amefunga mabao matatu, mechi hizo ni dhidi ya Coastal, TRA, Dodoma Jiji (hakufunga) na Tanzania Prisons.

Licha ya kufunga mabao hayo, Mwalimu akikosekana katika mchezi tatu kabla ya kurejea dhidi ya TRA, kufuatia kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 1 milioni kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Dodoma Jiji FC, Andy Bikoko wakati Simba ikitoka suluhu dhidi ya walima dhabibu hao.

Wakati Simba yenye pointi 34 katika nafasi ya pili ikihitaji kulipa kisasi dhidi ya Azam pia kupunguza tofauti ya pointi kati yao ya Yanga ambao wanaongoza kwa tofauti ya pointi nne, Mwalimu anategemewa kuwa silaha muhimu kwa kocha Steve Barker.

Tangu amalize adhabu yake katika mechi hizo mbili ambazo amefunga mfululizo, Mwalimu ametumika kwa jumla ya dakika 160 kati ya 180, katika mchezo dhidi ya TRA alicheza kwa dakika 70 huku dhidi ya Coastal akimaliza zote 90.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *