
Dar es Salaam. Wakati bei ya gesi ya kupikia (LPG) ikiendelea kupanda katika soko la dunia, kampuni ya Taifa Gas imesema haitapandisha bei ya nishati hiyo kwa watumiaji wa majumbani, ikilenga kulinda wateja dhidi ya makali ya ongezeko hilo.
Hatua hiyo inakuja kufuatia ongezeko la takribani asilimia 43 ya bei ya gesi ya kupikia katika wiki za hivi karibuni, hali iliyosababisha kupanda kwa gharama za ununuzi na usambazaji katika minyororo ya ugavi duniani.
Bei ya nishati hiyo imepanda kutokana na ongezeko la bei katika soko la kimataifa, hali iliyochangiwa na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Aprili 3, 2026, Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius amesema kampuni hiyo imeamua kubeba athari za ongezeko hilo ili kuhakikisha wateja wanaendelea kupata huduma kwa bei nafuu na uhakika.
“Katika mazingira haya ya sasa, tunayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wateja wetu kwa kubeba athari za ongezeko la gharama ya nishati ya kupikia kwa kutokuongeza bei huku tukihakikisha upatikanaji endelevu wa gesi safi na ya kuaminika,” amesema.
Ameeleza kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu kwa kaya nyingi na biashara ndogo ndogo nchini, hivyo uamuzi huo unalenga pia kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji.
Deogratius amesema Taifa Gas itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa gesi nchini kupitia mtandao wake wa maghala 25, unaohudumia maeneo ya mijini na vijijini, huku ikiendelea kuwekeza katika miundombinu ya usambazaji.
“Tanzania ni nchi kubwa yenye mahitaji tofauti, hivyo upatikanaji wa nishati hii ni kipaumbele chetu kikuu,” amesema.
Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuendelea kuunga mkono ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi, ikiwa ni pamoja na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, huku ikibainisha kuwa matumizi ya LPG yanachangia kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira.
Taifa Gas imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la kimataifa na kuchukua hatua stahiki kulingana na hali itakavyokuwa, huku ikiweka mbele maslahi ya wateja wake.
“Jukumu letu ni kuwalinda Watanzania kwa kuwapa huduma bora, uendeshaji wenye uwajibikaji na dhamira ya muda mrefu ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi nchini,” amesema Deogratius.