Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amesema wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) wanaendelea na jitihada za kurejesha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha Machi 24, 2026.

Akizungumza leo Aprili 4, 2026, Kyobya amesema barabara kuu ya Ifakara–Mlimba iliyokatika katika maeneo matatu imeanza kupitika kwa magari madogo, huku mabasi na malori yakiendelea kuzuiwa kutokana na kazi za matengenezo zinazoendelea.

Amesema uharibifu mkubwa umetokea katika eneo la Chita, ambapo wataalamu wameanza kazi ya kuweka miundombinu ya daraja ili kurejesha mawasiliano kikamilifu.

“Kwa sasa magari madogo yanaweza kupita katika baadhi ya maeneo, lakini kazi bado inaendelea. Tunatarajia hali itaimarika kadri matengenezo yanavyoendelea,” amesema Kyobya.

Treni ya reli ya Tazara inayosafirisha abiria kutoka Mlimba -Ifakara -Mlimba baada ya barabara ya Ifakara -Mlimba kukatika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Machi 24 na kufanya ishindwe kupitika kwa usafiri wa mabasi.

Wakati huohuo, usafiri wa treni maarufu kwa jina la ‘kipisi’ unaounganisha Mlimba na Ifakara umeendelea kuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo, ukiwezesha usafiri wa abiria na mizigo licha ya changamoto ya barabara.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Jamal Abdul, amesema huduma ya treni hiyo imekuwa muhimu kwa watumishi na wananchi kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki ambacho shughuli za maendeleo zinaendelea.

“Bila treni hii, tungekuwa tumekatika kabisa. Imetusaidia kusafirisha watumishi, vitendea kazi na hata kufanikisha maandalizi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ile ya mbio za Mwenge wa Uhuru,” amesema Abdul.

Hata hivyo, ameainisha changamoto zinazoendelea kujitokeza kutokana na kukatika kwa barabara hiyo, ikiwemo ugumu wa kusafirisha vifaa vya ujenzi kama saruji, bati na mbao, pamoja na bidhaa za chakula, kutokana na magari makubwa kushindwa kupita.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mlimba wameeleza kuwa treni ya ‘kipisi’ imekuwa msaada mkubwa katika kipindi hiki kigumu.

Mkazi wa Mlimba, Yusta Joachim, amesema treni hiyo imewawezesha kufika Ifakara kwa urahisi kwa ajili ya huduma mbalimbali, ikiwemo matibabu na biashara.

“Tumeweza kusafiri na kusafirisha mizigo ya chakula na bidhaa nyingine. Hata wagonjwa wanaohitaji rufaa wamekuwa wakitumia usafiri huu kufika Ifakara na kuendelea na safari,” amesema Joachim.

Ameongeza kuwa wanatumaini matengenezo ya barabara hiyo yatakamilika haraka ili kurejesha hali ya kawaida ya usafiri na usafirishaji katika wilaya hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *