
Unguja. Fedha za malipo kwa wanafunzi wa halaiki walioshiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zimezua sintofahamu, huku baadhi ya wazazi na wanafunzi wakidai kudhulumiwa, wakati Serikali ikitoa ufafanuzi kuhusu kilichojitokeza.
Takribani wanafunzi 1,000 wa shule za msingi na sekondari walishiriki mafunzo ya siku 30 kwa ajili ya halaiki ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru uliofanyika Aprili 2, 2026, katika Uwanja wa Gombani, Wilaya ya Chake Chake, na mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Katika picha za video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, wazazi na wanafunzi hao wameonekana wakidai kudhulumiwa fedha walizoahidiwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashi, amesema shutuma zinazotolewa ni tofauti na uhalisia.
Kwa mujibu wa wazazi hao, wanafunzi walitakiwa kupewa Sh300,000, lakini walipewa Sh150,000.
“Tunataka haki zetu, tunataka haki zetu… tunataka haki zetu,” hizi ni baadhi ya kauli zinazosikika katika video hizo zikiwaonesha wanafunzi hao wakikusanyika katika shule kisiwani Pemba.
Kauli ya Serikali
Katika taarifa kwa umma, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashi, aliyoitoa leo Aprili 5, 2026, amesema shutuma zilizotolewa ni tofauti na uhalisia.
“Baada ya uvumi huo, nachukua fursa hii kuwatarifu wazazi na walezi kwamba jambo hilo halina ukweli,mwongozo wa bajeti umeeleza wazi posho za watoto hao,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa mwongozo huo, kila mtoto alitakiwa kulipwa Sh150,000 kwa siku 30, ambapo kila siku kila mtoto analipwa Sh5,000.
“Machi 9, 2026, walilipwa Sh100,000, na Aprili 04, 2026 saa tano asubuhi, mhasibu alifika Shule ya Msingi Michakaini kulipa baki ya Sh50,000 kwa kila mtoto.
“Baada ya kufika katika kituo hicho na kuanza kulipa, walijitokeza wazazi na walezi walioambatana na watoto na kukataa kupokea malipo hayo kwa madai ya kwamba fedha walizostahiki kulipwa watoto hao kwa kila mmoja ni Sh300,000.”
Kwa mujibu wa maelezo ya mkuu wa mkoa, baada ya kutokea hali hiyo, walikaa na wazazi kuwaeleza ukweli ulivyo.
“Hata hivyo, tuliwajibu wazazi kwamba watoto wetu wanastahiki nyingine ni huduma ya chakula kwa siku za Ramadhani ambazo hawakuwa wakipewa chakula,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yake, “fedha hizo zipo, ila lazima waombe idhini ya kubadilisha fedha hizo kutoka chakula kwenda kwenye posho, ikiwa mamlaka husika itaridhia kubadilisha matumizi hayo.”
Ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi kuendelea kuwa wavumilivu na waridhie vijana wao wachukue posho hiyo iliyobakia ya Sh50,000 huku wakisubiri kupata idhini ya uhamishaji wa fedha hizo.
“Ninaahidi kwamba hakuna mtoto atakayedhulumiwa haki yake,” amesema Hadid.