
HADI raundi ya 12 mshambuliaji wa Yanga Princess, Jeaninne Mukandayisenga anaongoza kwenye msimamo wa wafungaji akiwa na mabao 18, huku akiacha maswali kama ataivunja rekodi ya Aisha Masaka?
Ikumbukwe nyota huyo raia wa Rwanda huu ni msimu wake wa pili kuitumikia Yanga na msimu uliopita aliingia dirisha dogo akifunga mabao 13 katika mechi tisa, hivyo amekuwa na mwendelezo bora wa ufungaji tangu alipojiunga na chama hilo akitokea Rayon Sports ya kwao Rwanda.
Zikiwa zimesalia mechi 10 kumaliza msimu na kwa kasi aliyonayo kinachosubiriwa ni kama nyota huyo ataweza kuifikia rekodi ya Masaka.
Masaka anayeitumikia Brighton ya England, msimu wa 2020/21 alifunga mabao 35 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake na hadi sasa idadi hiyo haijafikiwa.
Miongoni mwa waliowahi kuikaribia ni Asha Djafar aliyefunga mabao 27 msimu uliofuata na Jentrix Shikangwa alifunga mabao 17 msimu wa 2022/23, Aisha Mnunka aliyefikisha 20 msimu uliofuata na Stumai Abdallah msimu jana alipomaliza na mabao 28.