Dar, Zanzibar/mikoani. Uchu wa madaraka, ombwe la uwajibikaji nchini, malezi duni kwa watoto, amani na umoja ni miongoni mwa jumbe zilizotawala mahubiri ya viongozi wa dini katika makanisa mbalimbali, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.
Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi hao wa kiroho, Taifa limetawaliwa na woga, mambo yanayosababishwa na uchu wa madaraka, unaowafanya viongozi waogope kusema ukweli kwa hofu ya kuondolewa kwenye nafasi walizonazo.
Wakati baadhi wakisema hivyo, wengine wamewasihi viongozi wenzao wa dini kuwa na utaratibu wa kuwaita na kuwakosoa viongozi wa Serikali faragha, badala ya kuwananga hadharani kwa maneno machafu.
Wengine wametumia mahubiri hayo, kutoa ujumbe wa kudumisha amani na umoja, kuwaombea viongozi wakuu wa nchi waongoze vema, huku wakiwataka wazazi kusimamia malezi ya watoto kikamilifu.
Sikukuu ya Pasaka husherehekewa kila mwaka duniani, kuadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, tukio linaloashiria ushindi wa uhai dhidi ya mauti kwa waumini wa dini ya kikristo.
Viongozi hao wa dini, wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti, walipokuwa wakihubiri katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka kwenye makanisa wanayoyaongoza.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Augustino Shao
Ubinafsi, uchu wa madaraka
Katika mahubiri yake ya sikukuu hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Augustino Shao, amesema wananchi kwa sasa wanakosa matumaini kwa kuwa Taifa limetawaliwa na woga na hali ya kushindwa kuwajibishana.
Yote hayo, amesema yanasababishwa na ubinafsi na uchu wa madaraka, wengi wanaogopa kusema ukweli ili kulinda nafasi zao, wakidhani wakisema wataondolewa.
Jambo hilo, amesema linalipeleka Taifa katika hali ya hatari na kuwaacha wananchi bila matumaini ya kesho, akisisitiza furaha ya Pasaka haitakuwa na maana kama watu wote hawatashughulikia kuondoa giza la maovu katika jamii.
“Taifa letu hivi sasa linaishi katika kipindi kigumu, kilichotawaliwa na woga mwingi kwa kutowajibisha viongozi wengi kwa sababu ya ubinafsi na uchu wa madaraka, wengi wanalinda nafasi zao wakidhani wakisema ukweli wataondolewa,” amesema.
Ameeleza ni imani yake kazi ya kila kiongozi ni kulinda haki na amani ya Taifa na hasa katika kutatua shida na kero za watu, na si vinginevyo.
Askofu Shao, amesema viongozi wengi walipewa nafasi hizo kwa sababu waliaminika kwa weledi na elimu zao, waliaminika kuwa na hekima ya kuongoza lakini yanayotokea yanashangaza na kukatisha wananchi tamaa.
“Lakini, tunachokishuhudia kwa sasa ni woga wa kusema ukweli kwa hali halisi ya Taifa letu. Kiongozi makini ni yule anayesimamia haki na ukweli,” amesema.
Amesema wanaposema uchumi wa nchi unakua kwa asilimia sita lakini deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 13 kwa mantiki na akili ya kawaida unaona hakuna mwelekeo mzuri.
Alitoa mahubiri hayo akirejea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akisema kilichomo ndani ya ripoti hiyo hakitoi matumaini, kwani kila mwaka hesabu zinaonyesha ubadhilifu.
Amerejea maudhui ya ripoti hiyo ya mwaka wa fedha 2024/25, akisema imeonyesha hasara katika maeneo mbalimbali ikiwemo usambazaji dawa.
“Agizo la ufufuko wa Kristo leo ndugu zangu ni kusema ukweli haki na uadilifu na kutunza yote aliyotukabidhi na ndio maana ya ufufuko,” amesema.
Viongozi wasinangwe hadharani
Wakati Askofu Shao akiyasema hayo, Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Michael Hafidh, ametaka viongozi wa dini kuwajibika kwa kuwaita faragha na kuwaonya viongozi wa Serikali wanaokwenda kinyume, badala ya kuwananga hadharani.
“Lakini viongozi wenyewe wakubali kusikiliza yanayosemwa, siamini kwamba wakisikiliza haya yanaweza kutokea,” amesema.
Amesema ufufuo wa Pasaka unakumbusha watu kupendana kwa hiyo kila mmoja bila kujali itikadi zao wanatakiwa kupendana na kusaidiana.
Katika mahubiri yake aliyoyatoa wakati wa ibada hiyo iliyofanyika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Yosefu Dar es Salaam, Shemasi Papianus Rwelamila, amewataka waumini kusema na kuusimamia ukweli hata wanapokumbana na changamoto, ili kuishi misingi ya Yesu Kristo aliyekubali kusulubiwa kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu.
“Maisha hayo yanapaswa kuendelea wakati wote. Tusimamie ukweli hata katika nyakati ngumu, kama Yesu Kristo alivyofanya kwa ajili ya ukombozi wa watu wote,” amesema.
Askofu wa kanisa kuu Anglikana Jimbo la Morogoro, Godfrey Sehaba akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika Kwa ibada ya Pasaka kanisani hapo. Picha Hamida Shariff
Ujumbe wa amani
Katiba mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba, amewataka waumini kudumisha amani, upendo na mashirikiano kwa kuwa hayo, ndio msingi wa maendeleo ya nchi.
Kwa sababu Yesu Kristo alimwaga damu msalabani, amesema waumini wanapaswa kupendana na kushirikiana katika kuijenga nchi na sio kuchochea matendo maovu yasiyopendeza duniani na hata mbele za mungu.
Kwa upande wa Mchungaji wa Kanisa hilo, Kanoni Mafumbi, amesema Yesu Kristo aliposulubiwa msalabani alinyoosha mikono yote miwili akiashiria kuunganisha jamii zote hivyo waumini wanapaswa kuungana nyakati zote.
“Pamoja na kunyoosha mikono, Yesu Kristo pale msalabani alitamka neno la kiyahudi ‘sharom’ akimaanisha amani, hivyo nawataka Wakristo wenzangu tudumishe amani kwa kuwa ndio chanzo cha maendeleo ya nchi,” amesema.
Ujumbe wa Rais
Katika salamu zake za Pasaka kwa Watanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kuyakumbuka na kuyaenzi mafundisho na matendo ya huruma, upendo, msamaha na kujitoa kwa ajili ya wengine ya Yesu Kristo.
“Pasaka hii itukumbushe umuhimu wa kudumisha amani, kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, ili tuendelee kujenga Taifa lenye fursa kwa wote, ustawi na maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho,” ameandika.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa
Kutunza umoja
Kwa upande wa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amesema umoja wa Wakristo na Watanzania kwa ujumla ni muhimu kuutunza.
“Tumepita katika vipindi vingi vigumu, lakini tukamuamini Mungu ya kwamba yeye tuliyemuomba akawa nasi hata sasa tunaweza kusherehekea Pasaka pamoja,” amesema.
Ametaka Mungu ndiye atumainiwe, huku kila mmoja kwa nafasi yake aoneshe kwa vitendo katika kudumisha umoja wetu kama Wakristo, na kama Watanzania.
“Mambo yote yaliyo mazuri tusiyapoteze kwa gharama yeyote na kila mmoja katika nafasi yake anawajibika katika hilo kutokupoteza mambo mazuri tuyafufue na ndiyo maana ya Pasaka.
“Tusiwe watu wa kuleta hofu bali kuwatia moyo waliokata tamaa. Katika kufufuka maana yake hata yale tuliyoyaona yamekufa tumuombe Mungu yaendelee kuhuishwa yawe mapya,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kusini Kati, Askofu Hans Mwakabana, ameeleza umuhimu wa nafasi ya wanawake katika huduma ya Kristo, akisema ni kubwa akirejea waliokwenda kaburini kwa Yesu walikuwa kina mama.
“Pasiwepo kundi lolote linalowanyima nafasi wanawake katika huduma sio sawa kusema wanawake hawawezi kuwa maaskofu, wakuu wa kanisa, wakuu wa majimbo na nafasi nyingine nyingi, sio sahihi” amesema.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes, amewataka Watanzania kuwaombea viongozi wakuu wa nchi, ili waongoze kwa mapenzi ya Mungu na kudumisha amani, upendo na umoja wa kitaifa.
“Tuliombee amani Taifa letu la Tanzania, Rais wetu, Makamu wa Rais na wote wenye dhamana mbalimbali, sisi tulio chini yao tuongozwe na kutawaliwa kama Mungu apendavyo,” amesema.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani amewataka wazazi na walezi, wanapoadhimisha Sikukuu ya Pasaka, kuhakikisha wanaendelea kusimamia malezi na makuzi ya watoto.
Amesema baadhi ya watoto kutokana na kukosa malezi bora wamekuwa wakishindana na wazazi wao jambo ambalo ni kinyume na maadili.
“Leo hii baadhi ya watoto wanawaambia wazazi wao wangewahi wangeweza kuwazaa, wanashindana na wazazi wao wanakataa malezi na miongozo wanajiongoza wenyewe wanajiamini eti wamesoma ‘English Media’ kwa hiyo wanafanya watakavyo na baadhi ya wazazi wanawainamia ndio mwanangu umesoma,” amesema.
Askofu Amani, amesema jamii ina wajibu wa kumrudia Mungu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu ili watoto na vijana waweze kuishi maisha mema.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde, Mchungaji Dk Geoffrey Mwakihaba
Vita ya Mashariki ya Kati
Askofu wa Kanisa KKKT Dayosisi ya Konde, Dk Geoffrey Mwakihaba, amewaomba wananchi kuiombea dunia wakati huu wa vita inayoendelea Mashariki ya Kati ili iishe.
“Niendelee kuwasihi watu wote wenye mapenzi mema kuiombea dunia wakati huu inapopitia katika majanga haswa vita huko Mashariki ya Kati, tuiombee kanisa letu ili idumu kwenye wajibu wake wa kuwa nuru kwa watu wote,”amesema Askofu huyo.
Askofu Mkuu wa kanisa la Pentecoste Bible Fellowship church in Tanzania (PBFCT), Japheth Mapogo wakati akihubiri kwenye ibada ya pasaka Aprili 5, 2026 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete
Kwa upande wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecoste Bible Fellowship Church in Tanzania (PBFCT), Japheth Mapogo, amewataka Wakristo nchini kusamehe na kuachilia hata wanapokuwa kwenye dhiki na mateso, akisema kuwa huo ndiyo Ukristo halisi.
Akitoa mfano wa Yesu Kristo, amesema alipokuwa msalabani katika mateso, alimsamehe yule mhalifu aliyesulubiwa pamoja naye.
”Yesu mwenyewe alipokuwa msalabani pamoja na mateso aliyoyapata, lakini alimsamehe yule mhalifu mmoja aliyesulubiwa pamoja naye,” amesema.
Imeandikwa na Jesse Mikofu (Zanzibar), Tuzo Mapunda, Baraka Loshilaa, Sute Kamwelwe (Dar), Rachel Chibwete (Dodoma), Saddam Sadick (Mbeya) na Janeth Mushi (Arusha)