
Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini umebaini asilimia 92 ya watoto walio na umri wa miaka 13 hadi 17 hawawezi kutatua changamoto ndondogo zinazoweza kuwakabili.
Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na mfumo wa malezi ya kisasa unaohusisha shughuli nyingi kufanywa na wafanyakazi wa nyumbani na wazazi kutoona umuhimu wa kuwapa watoto wao kazi ndogondogo zinazojenga stadi za maisha.
Jambo hilo linatajwa kuwa na athari kwani zinajenga kizazi tegemezi na kinacholalamikia kila kitu wanachokifanya badala ya kutafuta suluhisho wanapokutana na changamoto.
Utafiti huo umefanywa na Uwezo Tanzania kati ya mwaka 2020 hadi 2023 kwa ushirikiano na mashirika mengine chini ya Regional Education Learning Initiative (RELI) katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zanzibar.
Kupitia utafiti huo, imebainika ni asilimia nane pekee ya watoto wenye umri huo Tanzania, ndiyo wenye uwezo wa kuona tatizo na kubaini njia tofauti zinazoweza kutumika katika kulitatua kwa ufanisi.
Kwa upande wa Kenya ni asilimia tano pekee ndiyo walikuwa na ufanisi huo, Uganda asilimia tatu na Zanzibar ikiwa kinara kwa asilimia 14.
Utafiti huo ulihusisha zaidi ya watoto 45,442 wa kike na wa kiume walio shuleni kutoka kaya 35,720.
Moja ya majaribio yaliyotumika ni kuwapima kama moto umetokea ndani ya nyumba yao ni tatizo na nini wanapaswa kufanya.
Utafiti huo unaonyesha mtoto wakubwa zaidi huonesha kiwango cha juu cha uwezo wa utatuzi wa matatizo ikilinganishwa na wa umri mdogo.
Kwa mfano, asilimia 6.5 ya watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 17 walikuwa na uwezo wa kubaini tatizo kwa kulichambua kutoka mitazamo tofauti na kujua kuwa lipo suluhisho. ikilinganishwa na asilimia 3.7 ya watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 14.
Elimu pia ina uhusiano na kuongezeka kwa uwezo huo kwani kwa wale wa sekondari asilimia 9.4 walikuwa na uwezo huo ikilinganishwa na asilimia 3.4 tu ya wale wa elimu ya msingi.
Nini sababu
Dk Daniel Marandu, mmoja ya watafiti katika program hiyo amesema hali hiyo inachangiwa zaidi na aina ya maisha ya sasa na malezi wanayopata watoto, yasiyokuwa na uwezo wa kuwajengea umahiri vizuri.
Hali hiyo inawafanya watoto kuwa na uwezo mdogo wa kutambua matatizo, kutafuta ufumbuzi na hata kukosa ushirikiano na kujitambua.
“Namna anavyokuzwa, kuanzia nyumbani shughuli anazopewa na wazazi, vitu anavyoambiwa kufanya havimjengei uwezo wowote. Watoto wengi wanalelewa na wadada wa kazi hapati nafasi ya kufanya kazi za mikono badala ya kupewa vitu vya kufikiria kuna mtu anafikiria kwa niaba yao,” anasema.
Anasema mfumo huu wa maisha umefanya sasa kila mzazi kumzingatia zaidi mtoto wake, tofauti na zamani mtoto alikuwa wa jamii nzima hivyo anapotoka nje hakuna wa kumsaidia.
Amesema wazazi wanapaswa kutambua michezo ya zamani ya maarufu kama ‘kimama-mama na baba’ iliyopotea sasa ni kwa sababu mazingira ambapo sasa watoto wanaangalia katuni na ‘gemu’ ambayo haimpi nafasi ya kukuza ubongo wake katika umahiri kwenye stadi za maisha.
“Kwa kawaida umri wa mwaka sifuri hadi minane ni kipindi kizuri cha mtoto kuchukua vitu vitakavyomjenga kwani akiwa mkubwa huendeleza kile kilichopo. Njia nzuri ya kukuza hali hiyo ni kumpa mtoto shughuli zinazoweza kumfanya achangamke afikirie,” amesema.
Amesema shughuli ambazo mtoto alikuwa akifanya zamani kama kusaidia kuosha vyombo au kupika zinapotea taratibu hali inayofanya hata uwezo wa watoto kufanya stadi za maisha kushuka.
Kizazi cha kulalamika
Amesema mzazi ndiyo anapaswa kuwa wa kwanza kukuza stadi hizo na mwalimu hupokea pale mzazi alipoishia na kukosekana kwa stadi hizo inatengeneza kizazi cha kulalamika katika kila kitu.
“Pia tunajenga kizazi tegemezi, zamani mtoto akimaliza darasa la saba au kidato cha nne ana akili ya kujitegemea lakini sasa mtu anamaliza chuo kikuu lakini uwezo wa kujitegemea au kutumia elimu yake kujitafutia kipato unakuwa upo kwa kiwango cha chini, hivyo tunatengeneza kizazi za kulalamika na kushindwa kujitegemea,” amesema.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Samwel Sitta ambaye ni ofisa programu mwandamizi kutoka Milele Foundation Zanzibar, amesema ushirikishwaji wa wazazi ni moja ya njia iliyotumika.
Kupitia program mbalimbali amesema wamekuwa wakiwafundisha wazazi namna ya kujenga stadi za maisha kwa watoto ili kupunguza utegemezi na kujenga kizazi chenye uwajibikaji.
Elimu hiyo imetolewa katika maeneo tofauti nchini na baadhi ya wazazi ambao walionekana kuwa na uelewa mzuri, wanatumika kama vinara kwa ajili ya kuwasaidia wengine.
Nini kifanyike
Ili kujenga uwezo wa watoto kumudu stadi za maisha na utatuzi wa matatizo, Dk Marandu anapendekeza kurudishwa kwa jando na unyago, michezo ya watoto, kibaba baba, kuruka Kamba na kombolela ilikuwa inawezesha kukuza ujuzi.
“Kwa mfano mchezo wa kibaba baba na mama, kuna mtoto wa kiume anajifanya baba na mwanamke anajifanya mama kuna kitu kinajijenga ndani yake, unapocheza kombolela ukijificha unatafutwa na wakati mwingine mchezo unasimama hadi upatikane ndiyo uendelee, hapa tunajenga uwezo wa kifikiri,” anasema.
“Kama tunaweza kurudisha michezo hii irudi, sasa hivi teknolojia inachofanya michezo imewekwa kidijitali lakini ujuzi unakuzwa kadri mtoto anavyochangamana, lakini anapojitenga ndiyo uwezo wa kukuza ujuzi unakuwa mdogo,” amesema.
Walichosema wazazi
Akizungumzia suala hilo, Mathayo Nelson, mkazi wa Kijichi jijini Dar es Salaam amesema bila kujua wazazi wamekuwa wakitengeneza kizazi tegemezi tangu wakiwa watoto wadogo hadi wanapokuwa.
“Sikuhizi utakuta hadi watoto wa miaka mitatu anapelekwa bweni, ambako ni vigumu kukuta mtoto anafundishwa shughuli ndogondogo kama kukata majani au kufagia, hii imekuwa ikifanya wengi wanaporudi nyumbani kuwa tegemezi.
“Wengine wakirudi nyumbani wazazi wanaona kama ndiyo muda wa wao kupumzika na hawawahusishi kwenye shughuli ndogo ndogo na hapo ndipo hadi nguo za ndani mtoto wa miaka 15 anafuliwa,” amesema.
Amesema umefika wakati sasa wazazi kupunguza usasa katika malezi ili kuhakikisha watoto wanakuwa wenye uwezo wa kutatua baadhi ya majukumu.
Maneno yake yanaungwa mkono na Mwanahawa Masha, pia mkazi wa Dar es Salaam ambaye anasema wazazi wengi wamekuwa wakishindwa kutafsiri neno malezi bora kwa watoto na kudhani kuwaondoa kufanya shughuli za nyumbani ndiyo njia inayotakiwa.
“Kwa sasa ni kawaida kukuta baadhi ya watoto wa miaka 12 hawawezi hata kujikorogea uji, hata kunyanyua ndoo yake ya maji akaoge hawezi,” amesema.
Amesema ni wakati sasa wazazi kurudi katika malezi ya Kiafrika ili kuhakikiha watoto wanakuwa na uwezo wa kujitegemea,” amesema.