Wapotoshaji habari mitandaoni sasa kukionaWapotoshaji habari mitandaoni sasa kukiona

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Protabas Katambi amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Camillus Wambura kuchukua hatua kali kwa wote wanaotoa taarifa za uzushi kupitia mitandao ya kijamii.

Katambi ametoa maagizo hayo katika soko lilioungua la Simu 2000 wilayani Ubungo Dar es salaam alipokuwa akitolea ufafanuzi baadhi ya mambo kuhusiana na moto na mengineyo yahusuyo ulinzi na usalama.

Akizungumza katika mkutano huo Katambi alisema hawatovumilia taarifa zozote za uzushi kuhusu viongozi, iwe taarifa za uzushi kuhusu taarifa za kiuchumi, zisizotafitiwa na zinazopelekewa kuvunja amani, kuondoa ushirikiano, usalama na mshikamano wa Watanzania.

Ameeleza hayo akihusisha taharuki iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu upotevu wa nyeti za wanaume kwa kushikwa bega ambazo zilianza kutokea katika mikoa ya Songwe na Mbeya, huku watu saba wakipoteza maisha kutokana na suala hilo.

Amesema serikali kupitia Jeshi la Polisi ilifanya uchunguzi wa kina na waliodai kuwa ni waathirika wa kupoteza viungo walifanyiwa uchunguzi wa macho na kitabibu na kubainika kuwa taarifa hizo si za kweli ni uzushi. SOMA: Aiomba TCRA kutoa elimu matumizi mitandao ya kijamii

“Jeshi liliwachukua hao wahusika au waathirika na kuwapeleka kwenye vyumba maalumu kufanya ukaguzi, walifanyiwa uchunguzi na ukaguzi kwa macho ya nyama na kitaalamu na kubainika kuwa nyeti hizo zipo na hivyo ni uzushi na ni uongo ambao umesababisha kupoteza maisha ya watu,” alisema Katambi.

Amesema uzushi huo ni kama mauaji yaliyotokea kwa watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino ambao ni mila potofu na ni uzushi unaoleta madhara makubwa kwa Watanzania.Katambi amesema huo ni uzushi ambao unahitaji kukemewa kwa sura zote za kidini, kimila lakini pia kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kusimamia sheria.“Kama waziri mwenye dhamana natoa karipio kali kwa wananchi wote ambao wanazusha mambo hayo.

Kwa wale wote wanaojichukulia sheria mkononi tutachukua hatua kali na hatutasita kufanya hivyo kwa sababu tunaenda kuathiri maisha ya watu na wako ambao wanapigwa, wanapata ulemavu kwa kitu ambacho ni cha uzushi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii,” alieleza Katambi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *