Katika Ukanda wa Gaza, pamoja nah atua ya kusitishwa mapigano tangu mwezi Oktoba mwaka jana, mashambulizi ya anga, mizinga na risasi yaliendelea katika maeneo mbalimbali, yakiripotiwa kusababisha vifo na majeruhi. Kwa ujumla, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, hadi kufikia mwezi uliopita, Machi, jumla ya waliouawa tangu kutangazwa kwa usitishaji mapigano wamefikia 689 na majeruhi 1,860.

media:entermedia_image:826ebed1-9f79-410e-aab6-1a8e904d59e0

Hospitali kuu ya Al-Shifa katika ukanda wa Gaza

Ndani ya Hospitali ya Al-Shifa, mojawapo ya hospitali kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza, athari za vita zinaonekana kila kona. Ni vigumu mimi kukupa picha kamili kama video tutakayoichapisha katika mitandao yetu ya kijamii ya Youtube wa Habari za UN na wavuti wetu news.un.org/sw lakini ni wazi hali ni tete kuanzia uharibifu wa majengo na miundombinu mingine hadi kupungua kwa uwezo wa kutoa huduma kutokana na uhaba wa umeme, vifaa na dawa. Hata magari ya kubebea wagonjwa yanaonekana yameharibika kiasi cha kutowezekana kutengenezwa tena.

Daktari Hassan Al-Shaer, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Al-Shifa, anasema janga la afya haliishii tu tena katika kupokea majeruhi pekee, bali sasa mikondo yote ya tiba hasa matibabu ya saratani.

“Kuna changamoto kubwa kwa wagonjwa wa saratani, kwani dawa zimekuwa adimu sana, na zile zinazopatikana hazizidi asilimia 15 ya dawa zote wanazohitaji wagonjwa hawa. Pia kuna matatizo mengine ya kimazingira. Sasa tunaanza kukumbwa na tatizo la panya pamoja na hatari za kiafya zinazoweza kutokea kutokana na hilo, kwa sababu ya mkusanyiko wa mamia ya maelfu ya tani za vifusi na maelfu ya tani za taka zilizotapakaa katika Jiji la Gaza.”

Kutokana na idadi kubwa ya vituo vya afya kutotoa huduma au kufanya kazi kwa kiwango kidogo, baadhi ya shule na makazi ya muda yamegeuzwa kuwa vituo mbadala vya tiba vinavyotoa huduma za msingi kabisa kwa watu waliokimbia makazi yao na wakazi wengine.

Mvulana kijana wa Kipalestina amesimama barabarani katikati ya magofu ya nyumba zilizoharibiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Al Shati katika ukanda wa Gaza, kufuatia mashambulizi ya anga.

© UNICEF/Mohammad Ajjour

Mtoto akicheza mtaani huku kukiwa na vifusi vya majengo yaliyobomolewa kwa mashambulizi kutoka angani kwenye kambi ya wakimbizi ya Al Shafi Ukanda wa Gaza.,

Katika moja ya shule za UNRWA  ambayo sasa inatumika kwa wakati mmoja kama makazi ya wakimbizi na kliniki ya matibabu; wagonjwa hupanga foleni kila siku kupata matibabu ya msingi, hali inayoonesha kwa dhahiri ukubwa wa janga linaloikabili sekta ya afya.

Mahmoud Al-Najar, mzee kutoka kambi ya wakimbizi ya Al-Shati, magharibi mwa Jiji la Gaza, anasema analazimika kutembelea kituo hiki cha matibabu karibu kila siku kutokana na magonjwa sugu, huku kukiwa hakuna hospitali zinazofanya kazi au upatikanaji wa matibabu anayohitaji.

“Nimekuja katika kituo hiki cha matibabu kupata tiba, na huja hapa kila siku kwa sababu hakuna hospitali katika Ukanda wa Gaza au hapa katika kambi ya Al-Shati. Kituo hiki kinatoa matibabu ya muda tu, na tunapokuja hapa wanatupa Panadol kwa sababu hakuna dawa nyingine, na hiyo ndiyo pekee wanayoweza kutoa. Hakuna hata Gazi. Ikiwa mtu amejeruhiwa, tunaomba madaktari watoe matibabu, lakini hawawezi kufanya hivyo.”

Katika hali kama hii wagonjwa wengi wanakabiliwa na kifo wakikiona lakini hakuna la kufanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *