Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu za Bongo, Zaiylissa amesema kwa sasa anaamini sana ndoa kama njia sahihi ya maisha yake kuliko mahusiano ya muda mfupi yanayosababisha  matatizo na kufanya mambo mabaya.

Zaiylissa ambaye amewahi kuwa kwenye uhusiano na Haji Manara, anasema kuzini ni moja ya mambo ambayo hayapendi na ndoa kwa sasa inampa heshima, ina mipaka yake na baraka zake baada ya kupitia mengi.

Akizungumza na Mwananchi alisema japo yuko kwenye ndoa na mumewe anayejulikana kama Said,  hapendi kumweka hadharani na kufunguka sababu za kumficha.

Anasema amechagua kuishi maisha ya faragha zaidi ili kulinda ndoa yake mpya dhidi ya changamoto za nje.

Sababu ya kuficha mume wake

“Nimejifunza kutokana na  makosa yangu ya nyuma, nilikuwa na tabia ya kuweka kila kitu hadharani, lakini haikusaidia lolote zaidi ya kuniumiza na kuwapa faida watu ambao hawakuwa na umuhimu wa kufahamu mambo yangu binafsi, sasa nimeamua kulinda kile nilichonacho, siyo kila kitu lazima kiwekwe mitandaoni ili kuthibitisha kuwa ni cha kweli.

Kwa wenye kumfahamu mume wangu Said ni watu wangu wa karibu tena pale nitakapokuwa naye kwa wakati huo, na siyo kumposti kwenye mitandao ya kijamii, hii ndio ‘system’ yangu mpya ya maisha, na sitarudi nyuma,” anasema Zaylisa.

Ameongeza hata siku akiamua kumposti mume wake, haitakuwa kwa sura nzima:

“Siku nikihisi kumposti, basi nitamposti nusu sura au mkono tu, hiyo inatosha kuonyesha uwepo wake bila kuingilia faragha yake kwa sasa maisha yangu si show off kwa  kila mtu.”

Mtazamo wake kuhusu ndoa

Pia aligusia suala la mahusiano na kuweka wazi msimamo wake kuhusu ndoa yake.

“Mimi ninaamini sana kwenye ndoa kuliko mahusiano ya muda mfupi au kuzini, ndoa ina heshima yake, ina mipaka yake na baraka zake, nimepitia mengi, lakini bado naamini ndoa ndiyo njia sahihi ya maisha, kiufupi napenda ndoa kuliko kuzini.”

Historia ya ndoa zilizopita

Hii ni ndoa ya nne baada ya ndoa zake tatu zilizopita kuvunjika kwa sababu tofauti, ndoa yake ya kwanza ilikumbwa na tuhuma za ukatili na alidai mume wake alikuwa akimpiga, ndoa ya pili ilikuwa na msanii wa singeli, Dulla Makabila, lakini haikudumu zaidi ya miezi mitatu.

Baadaye aliolewa na Haji Manara, ambaye aliwahi kuwa Ofisa Habari wa klabu za Simba na Yanga, lakini ndoa hiyo pia ilivunjika baada ya miezi minne tu.

Ndoa mpya na sherehe ya kifahari

Zaylisa alifunga ndoa na Said Februari 16, 2026, na juzi, Machi 27, 2026, aliandaa hafla maalum ya “usiku wa chai” iliyohudhuriwa na mastaa mbalimbali wa burudani nchini, ikiashiria mwanzo mpya wa maisha yake ya ndoa.

‘System mpya’ ya maisha kwa sasa, anaonekana kubadilika kabisa na kuanza ukurasa mpya wa maisha, mashabiki wake wengi wanaona huu ni uamuzi wa busara, hasa baada ya kupitia changamoto nyingi kwenye mahusiano yake ya nyuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *