Mji wa Iten, unajulikana kote duniani kama “Nyumbani kwa Mabingwa,” ni kituo maarufu cha mafunzo katika mwinuko wa juu wa ardhi kwa wanariadha nguli wa mbio za masafa marefu, lakini eneo hilo lililokusudiwa kulea vipaji, nidhamu na ubora, limegeuka kuwa la ukatili na mauaji.

Kwa mujibu wa UNFPA nchini Kenya, asilimia 69 ya wanawake katika michezo wamewahi kukumbana na ukatili wa kijinsia, au wanajua mtu aliyewahi kukumbana nao. Hizi si takwimu tu, zinaakisi hali halisi ndani ya mfumo ule ule unaozalisha mabingwa.

Mwanamume wa Kenya amevaa mavazi ya michezo akizungumza wakati wa mahojiano ya nje yanayohusiana na mipango ya UNFPA ya uhamasishaji dhidi ya GBV.

Kocha, Richard Kanda asema shughuli za michezo zinazoungwa mkono na UNFPA nchini Kenya husaidia kuzuia ukatili wa kijinsia.

Kocha, Richard Kanda, akiwa sehemu ya jamii ya wanariadha, anaelewa kuwa mafanikio ya uwanjani hayawezi kutenganishwa na ulinzi wa mwanariadha. 

“Sasa kuna changamoto tulikuwa tunakabiliana kuhusu GBV, zilienea kila mahali hapa Iten. Kambi yangu ndio tulikuwa tumeathirika wakati mkimbiaji wetu mmoja alipouawa. Baada ya kupewa mafunzo ya Kujilinda, sasa tutazuia jambo kama hilo lisitendeke tena katika kambi yetu.”

Kutokuwepo kwa usawa wa madaraka na ukosefu wa mifumo ya uwajibikaji kunawaacha wanawake vijana katika mazingira hatarishi zaidi ya kufanyiwa unyanyasaji. Mwanariadha, Gladys Chemutai, anasimulia.

“Ukiwa mwanariadha wa kike unakumbana na changamoto nyingi. Kama hausaidiwi na familia yako, utajiingiza kwenye mahusiano na kuzoeana na baadhi ya makocha, wanakwambia tutakusaidia ili changamoto zako zikome. Unapotaka kutoka kwenye hayo mahusiano sasa hapo ndiyo anapata changamoto kwa yule anayemkataa na hapo ndio unaona GBV inaanza sasa.”

Kwa msaada wa UNFPA, makocha, wanariadha na maafisa wengine wa michezo wanapokea elimu ya ulinzi kuhusu utambuzi, uzuiaji na ukabilianaji wa ukatili wa kijinsia. Kocha Kanda anasema.

“Mafunzo ya Kujilinda yanatusaidia sana, tunahakikisha mahali walipo panakuwa na mazingira salama na rafiki. Kila mtu kwenye kambi anajua ni nini afanye. Sisi sasa kama makocha ndio tunashikilia tuone kila kitu kambini kimeenda vizuri, wakimbiaji wanafurahia mazingira na hata hao wafanyakazi wengine wanafurahia mazingira.”

Miongozo ya wazi sasa imeanzishwa katika kambi za mafunzo ya riadha na kuimarisha mifumo ya kutoa taarifa, na uwajibikaji ambapo kukaa kimya si jambo la kawaida tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *