Tarime. Serikali imewaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kutumia nyumba za ibada kuhimiza amani, mshikamano, upendo na umoja katika jamii ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya maendeleo katika mazingira tulivu.

Wito huo umetolewa Aprili 11, 2026 mjini Tarime na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, wakati wa harambee ya ujenzi wa ofisi ya Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Jimbo la North Mara Field.

Katika harambee hiyo, Dk Nyansaho aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema zaidi ya Sh640 milioni zilichangwa, huku yeye na msafara wake wakichangia Sh82 milioni.

Akizungumza kabla ya harambee, Dk Nyansaho amesema nyumba za ibada zina mchango mkubwa katika kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa, akibainisha kuwa mafundisho ya dini zote yanahimiza maadili hayo.

New Content Item (4)

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Dk  Rhimo Nyansaho akizungumza kwenye harambee ya ujenzi wa ofisi ya kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) jimbo la North Mara Field wilayani Tarime.  Picha na Beldina Nyakeke

“Mafundisho haya ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kutekeleza majukumu yake na kuleta maendeleo endelevu. Viongozi wa dini ni wadau muhimu katika kufanikisha hilo,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Dk Nyansaho pia ametaja mchango wa SDA katika sekta ya elimu mkoani Mara tangu mwaka 1913, akisema umechangia kuinua maisha ya wananchi, akiwemo marehemu Profesa Philemon Sarungi na Profesa Samuel Wangwe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo, ameomba msaada wa Serikali kuu katika upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Tarime–Mugumu ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

Awali, Askofu wa SDA Jimbo la North Mara Field, Dk Benjamin Biha, amesema ujenzi wa jengo la ofisi la ghorofa mbili unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh3.5 bilioni.

Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili, lengo likiwa kusogeza huduma za kiroho karibu zaidi kwa waumini baada ya kugawanywa kwa jimbo hilo kutoka Jimbo la Mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *