Dar es Salaam. Wapenzi wa muziki wa miaka ya 1960 mwanzoni watamkumbuka mwanamuziki aliyetamba miaka hiyo aliyeitwa Edward Masengo. Huyu mwanamuziki asili yake ilikuwa Kongo, lakini alikuja kufahamika sana Afrika ya Mashariki kutokana na nyimbo zake nyingi kuwa ni za Kiswahili, na zilikuwa na hadithi za kusisimua na hata vichekesho vya kuvunja mbavu. 

Edward Mazengo kama ilivyokuwa nduguye John mwenda Bosco walikaribishwa Kenya na Peter Colmore, Muingereza aliyekuwa na kampuni yake ya ‘promotion’ aliyoiita High Fidelity productions Limited, kampuni iliyokuwa ikitangaza bidhaa mbalimbali zilizokuwa zikitengenezwa Kenya.

Nyimbo zao za matangazo kama vile Aspro ni dawa ya kweli, Sanyo Juu, Sanyo top of the pops, ziliimbwa na wakubwa na watoto.  Lakini kubwa zaidi ilikuwa nyimbo zao, leo nimgusie zaidi Edward Mazengo na nyimbo zake.

Wimbo wake wa kwanza alioutunga baada ya kuingia Afrika Mashariki ulikuwa ukilalamika tofauti za mambo mengi kati ya nchi alikotoka na alipokuwa. Katika wimbo huo ulifahamika zaidi kama ‘Kumbe safari kweli tabu’ alikuwa akilalamika jinsi kitu kimoja kilivyoweza kuwa na majina mawili tofauti. Edward aliimba hivi,

Kumbe safari kweli tabuu,
Tulikuwa kwetu Kongo,
Tunatembea kuume
Tukaja Nairobi, Tunatembea kushoto,
Kukongo twala ugali,
Uganda wala matoke.
Nairobi wala Ugali
Tumbo nayo ni matata,
Kukongo ni faranga,
Nairobi ni shilingi.

Wimbo wake mwingine uliokuwa kati mtindo huo huo aliuita Maswahili Inaachana, ulikuwa na maneno haya,
Mi nasema kuja hapa, waao wanasema njoo hapa,
Niliomba na lupawa nilitaka kula mchele,
Wao wanasema unataka kula wali,
Kisha nikasema naomba lupawa,
Wao wanasema hii ni kijiko

Kuna nyimbo zake zilikuwa zinachekesha, kama ule uliokuwa ukiitwa . Pilipili yasipokula inakuwasha namuna gani. Wimbo huu ulikuwa ukizungumzia watu wanaopenda kuchonganisha ndoa za watu. Wimbo wake Ulofa ni mbaya sana sana, ulikuwa na maneno haya ulikuwa na maneno ya kuchekesha pia, 

Ulofa nao ni kitu mubaya sana ,Hautakula hautavala sana sana.
Wimbo mwingine ulikuwa Bembeleza mapendo kwa bwana upate pesa, ulikuwa ni ushauri kwa wanawake baadhi ya maneno yalikuwa,

Bembeleza mapenzi kwa bwana upate pesa,
Kama uko na kiburi kwa bwana hakuna pesa.
Wimbo ambao hakika ulichekesha sana watu ni ule aliouimba na kuigiza kama Analia, ulikuwa na maneno yafuatayo;

Watu usiku hulala, mimi huketi nalia
Nikimukumbuka mpenzi maneno aliyonambia.
Mpenzi wangu nakuwaza, mpenzi wangu nakulia,

Kilichochekesha katika wimbo huu ni namna alivyouimba, alianza kwa kuimba vizuri aliporudia beti hiyo akaanza kuimba huku analia kutokana na maneno yale aliyoambia na mpenziwe.
Edward Mazengo ni kati wa wapiga magitaa makavu waliong’aa sana mwishoni mwa miaka ya 50 na mwanzoni mwa miaka ya 60.

Alipendwa sana Tanzania kiasi cha kuweza kurekodi na mkongwe mwingine wa zama hizo, Frank Humplick mwanamuziki maarufu aliyekuwa mkazi wa Moshi wakati huo.Edward Mazengo aliwahi hata kukaribishwa nyumbani kwa Mwalimu Nyerere enzi hizo.

Kama nilivyosema hapo juu Mazengo alikuwa mmoja wa wapiga magitaa makavu wa enzi hizo. Magitaa makavu ilikuwa ni mtindo wa kupiga magitaa yaliyokuwa hayatumii umeme.

Na mpigaji mara nyingi alikuwa mmoja na alikuwa anauwezo wa kupiga ukaweza kusikia bezi na solo katika wimbo wake. Kampuni ya Galotone ya Afrika ya Kusini ilirekodi wapigaji wengi wa aina hii ya upigaji Afrika ya Mashariki kabla ya uhuru, na kampuni hiyo pia ilikuwa ikiuza magitaa ambayo yalikuwa na lebo ya Galotone, mpaka siku hizi wanamuziki wengi huyaita magita yasiyotumia umeme ‘Magalatoni’.

Karibu nchi nzima kulienea wapigaji wa magitaa makavu, walikuwa watumbuizaji maarufu sana kwenye vilabu vya pombe, na kuna wengi walipata bahati ya kurekodiwa nyimbo zao na Radio Tanzania, na wengine kupata umaarufu mkubwa kama vile marehemu Mzee Kungubaya ambaye wimbo wake ulikuwa maarufu kutokana na kufungua na kufunga kipindi cha Salamu za Wagonjwa enzi hizo katika radio ya Taifa.

Nyimbo zilizopigwa na marehemu baba yangu kwa mtindo huo wa gitaa kavu na kurekodiwa mwaka 1978, zimepata nafasi ya kufufuka tena kwani santuri za nyimbo hizo zitaanza kusambazwa tena na kampuni ya Mississipi Records. Nami niko mbioni kurekodi nyimbo chache kuendeleza mtindo huo wa gitaa kavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *