Dar es Salaam. Katika kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapenda masomo ya sayansi, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), kimetoa mafunzo kwa wanafunzi 35 kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Sega, iliyopo mkoani Morogoro.

Fursa hiyo ya kipekee wamepata wanafunzi hao katika Chuo Kikuu cha Aga Khan jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wanafunzi hao wakiwa chuoni hapo walipata fursa ya kujifunza kwa kina masuala ya sayansi yanayogusa maisha yao ya kila siku na mustakabali wao wa kitaaluma.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanafunzi hao kuyaona masomo ya sayansi nje ya darasa kupitia uzoefu halisi unaohusisha afya ya akili, matumizi ya teknolojia katika sayansi, uuguzi, kujitambua pamoja na elimu ya hedhi salama.

New Content Item (4)

Kupitia programu hiyo, wanafunzi wamejifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu na wahadhiri wa chuo hicho, jambo lililoongeza hamasa yao ya kuendelea na masomo ya sayansi.

Akizungumza na Mwananchi Digital chuoni hapo, Mshauri wa wanafunzi kutoka shule hiyo, Jane Myombo amesema lengo la kuwapeleka wanafunzi hao chuoni hapo ni kuwajengea uelewa mpana na kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi kwa kuyaona kwa vitendo kutoka kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu hasa wa Chuo Kikuu Aga Khan, badala ya kubaki kwenye nadharia pekee.

“Tumewaleta hapa ili waone kwa vitendo kile wanachojifunza darasani. Hii itawasaidia kuongeza hamasa, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi ya taaluma zao za baadaye,” amesema Myombo.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wanafunzi kujitambua mapema na kuchagua taaluma zinazolingana na uwezo na vipaji vyao, jambo litakalowasaidia kuwa na mwelekeo sahihi wa maisha ya baadaye.

“Binafsi ninaamini hii ni fursa ya pekee kwao kukutana na watu waliosoma masomo kama yao wakiwa kidato cha nne na sasa wamefanikiwa kufika chuo kikuu wakipambania walichokiamini bila kujali jinsia zao. Hii itawapa hamasa ya kujifunza zaidi wakiamini kama wenzao wameweza na wao wataweza pia.”

“Kwani pamoja na mambo mengine wamefundishwa kujitambua ambalo ni jambo la msingi, ukitaka kutimiza malengo yako kwanza ujue wewe ni nani na unataka nini kwa ajili gani,”amesema Myombo.

New Content Item (4)

Mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka shule hiyo Patricia Mwaipyana, aliyeshiriki mafunzo hayo, amesema amejifunza umuhimu wa kujitambua, akieleza kuwa mtu akijitambua anaweza kujisaidia na hata kuwasaidia wengine.

“Nimejifunza kwamba ukijitambua, unaweza kujisaidia na kuwasaidia wengine pia. Pia nimeelewa mambo ya kuzingatia kabla ya kuchagua kazi, hasa kuchagua kile ninachokielewa zaidi,” amesema mwanafunzi huyo.

Naye mwanafunzi mwingine, Lisamanu Mapinduzi amesema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwake katika kumsaidia kubaini taaluma inayomfaa kulingana na uwezo na masomo anayoyasoma.

“Mafunzo haya yamenisaidia kuelewa ni kazi gani inanifaa kulingana na sifa zangu. Pia nimejifunza namna ya kukabiliana na changamoto za hedhi ili nisiache masomo, pamoja na jinsi ya kushughulikia changamoto za afya ya akili ambazo kwa sasa zimekuwa kubwa kwa vijana,” amesema Lisamanu.

Kwa upande wake, Peter Mangi, Ofisa wa Uandikishaji Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan, amesema mafunzo waliyoyapata wanafunzi hao yanalenga kuwajengea  msingi imara wa kitaaluma na kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi.

“Tumewapatia mafunzo mbalimbali ikiwamo kujitambua, afya ya akili, matumizi ya teknolojia na namna ya kuchagua taaluma sahihi. Mafunzo haya yametolewa na wataalamu na wahadhiri wa chuo ili kuwajengea uelewa wa kina,” amesema.

Mafunzo hayo yamekuja wakati ambapo juhudi zinaendelea kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika masomo ya sayansi, yakionekana kuwa nyenzo muhimu ya kuwaandaa vijana wa kike kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa na kuchangia maendeleo ya jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *