Katika ujumbe wake leo kwa Kikao cha Tano cha Jukwaa la Kudumu la Watu wenye Asili ya Afrika kilichofanyika Geneva, Uswisi kiongozi huyo amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi hayawezi kutenganishwa na juhudi pana za kulinda haki za binadamu na heshima ya utu.

Amebainisha kuwa watu wenye asili ya Kiafrika bado wanakumbana na dhuluma nyingi duniani, nyingi zikiwa zimejikita katika historia ya utumwa, ukoloni, na unyonyaji. Ameongeza kuwa dhuluma hizi za kihistoria bado zinaonekana katika mifumo na taasisi za sasa ambazo zinahitaji mageuzi ya haraka.

“Haki za watu wenye asili ya Kiafrika zinakiukwa mara kwa mara na mara nyingi kwa uwazi,” ujumbe huo umesema, ukirejelea pia aina fiche za ubaguzi ambazo huacha athari za kudumu kijamii na kiuchumi. Ukosefu wa usawa katika mamlaka, rasilimali, na fursa unaendelea kufuata misingi ya rangi, ameonya.

Katibu Mkuu amesifu ajenda ya jukwaa hilo kwa kushughulikia masuala muhimu kama haki za fidia, uwajibikaji wa taasisi, uwezeshaji wa vijana, na ulinzi wa urithi wa kitamaduni. Ameeleza jukwaa hilo kuwa “jukwaa muhimu” katika kuleta mabadiliko yenye maana.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa Muongo wa Pili wa Kimataifa wa Watu wenye Asili ya Kiafrika, kipindi kinacholenga kukuza utambuzi, haki, na maendeleo kwa jamii hizi duniani. Katibu Mkuu amezitaka nchi zote kutekeleza kikamilifu Makubaliano ya Durban na Prorgramu ya Hatua, mfumo muhimu wa kimataifa wa kupambana na ubaguzi wa rangi.

Akitoa wito wa “hatua za ujasiri,” mesisitiza umuhimu wa serikali na taasisi kuongeza juhudi za kuondoa ubaguzi wa rangi katika aina zote na kuhakikisha heshima kamili ya haki za watu wenye asili ya Kiafrika.

Amehitimisha kwa wito wa mshikamano wa pamoja ili kujenga mustakabali wenye heshima, usawa, na haki si tu kwa watu wenye asili ya Kiafrika, bali kwa dunia nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *