Ripoti hiyo imetolewa leo jijini Khartoum, Sudan na UNDP kwa kushirikiana na Taasisi ya Masuala ya Usalama, (the Institute for Security Studies, ISS), ikiwa na uchambuzi wa kwanza wa aina yake kutoa mwelekeo wa muda mrefu tangu kuanza kwa vita Aprili 15, 2023, ukiainisha gharama za miaka mitatu iliyopita na hasara zitakazotokea ikiwa vita vitaendelea.

Uchambuzi huo mpya unaonesha kuwa tayari Sudan imepoteza dola bilioni 6.4 za pato lake la taifa ndani ya mwaka 2023 pekee huku karibu watu milioni 7 wakitumbukia kwenye umaskini uliokithiri ndani ya mwaka mmoja tu. Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Sudan, Luca Renda, ameelezea hali hiyo akisema, “miaka mitatu ndani ya mzozo huu, hatukabiliwi tu na janga, tunashuhudia mmomonyoko wa kimfumo wa mustakabali wa nchi. Takwimu hizi si namba tu za kufikirika; zinaonesha familia zilizosambaratika, watoto walio nje ya shule, riziki zilizopotea, na kizazi ambacho matumaini yake yanazidi kufifia kila kukicha.”

Halima, mwenye umri wa miaka 30, anamshikilia binti yake wa miezi sita, Samira, ambaye ana sindromi ya Down na hivi karibuni alitibiwa kutokana na utapiamlo, ndani ya hema katika kambi ya wakimbizi huko Tawila, Darfur ya Kaskazini, Sudan.

© UNOCHA/Giles Clarke

Kwa sasa, mapato ya wastani nchini Sudan yameshuka hadi kufikia kiwango ambacho kilionekana mara ya mwisho mwaka 1992, huku viwango vya umaskini vikiwa vibaya zaidi kuliko miaka ya 1980. Ripoti hiyo inaonya kuwa ikiwa vita vitaendelea, kufikia mwaka 2043 pato la taifa litakuwa chini kwa dola bilioni 34.5 ikilinganishwa na hali ambayo ingekuwepo bila vita, huku pato la wastani la kila mtu likipungua kwa takriban dola 1,700. 

Umaskini uliokithiri utazidi asilimia 60 ya idadi ya watu, idadi ambayo ni sawa na watu milioni 52, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 34 zaidi ya ambavyo ingekuwa bila vita, ongezeko ambalo ni kubwa kuliko jumla ya watu wote nchini Ghana.

Suluhisho la kurejesha maendeleo na amani nchini sudan

Ripoti hiyo inabainisha kuwa, hata kama vita vitaisha mwaka huu 2026, urejeshaji wa uchumi utakuwa wa taratibu sana, huku ukuaji wa uchumi ukikadiriwa kuwa asilimia 1.2 pekee. Hata hivyo, kuna mwanga wa matumaini kupitia mfumo wa “Sudan Rising” ambapo amani ikipatikana na mageuzi ya utawala, kilimo, afya, na miundombinu yakifanyika, pato la taifa linaweza kufikia dola bilioni 58.2 ifikapo mwaka 2043. Chini ya mpango huo, watu milioni 17.3 wanaweza kuondolewa kwenye umaskini wa kupindukia na umri wa kuishi unaweza kuongezeka kwa miaka 4.2.

Luca Renda amesisitiza kuwa nafasi ya kupata mafanikio haya inazidi kupotea kadiri muda unavyokwenda, na kutoa wito wa dharura wa amani, “takwimu zinaonesha kuwa bado inawezekana kuikwamua Sudan, lakini kila mwezi unaopita mzozo ukiendelea, inafanya kazi hiyo kuwa ngumu zaidi na yenye gharama kubwa zaidi. Maamuzi yanayofanywa sasa ndiyo yataamua ikiwa hali ya Sudan inaweza kurekebishwa au la.”

Ripoti hiyo inahitimisha kuwa bila hatua za haraka kurejesha utulivu, Sudan itashuhudia miaka mingine mingi ya kudorora kwa uchumi na kupoteza maendeleo yaliyopatikana kwa miongo kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *