Kupitia video yake aliyochapisha kwenye ukurasa wa X, zamani Twitter, Dkt. Tedros anasema katika bara la Amerika, ugonjwa huu huambukizwa na wadudu, “lakini duniani kote mara nyingi huambukizwa wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua.”

Anasema ni kwa mantiki hiyo, WHO imeamua mwaka  huu maudhui ya siku hii yawe Wanawake ni kitovu, linda kizazi kijacho dhidi ya ugonjwa wa Chagas.

 Dkt. Tedros ameeleza kuwa ugonjwa huu unaweza kuzuilika na kutibika miongoni mwa wanawake na watoto wacahnga waliozaliwa.

“Hata hivyo bado wanawake wengi hawafanyiwi uchunguzi au wanakumbwa na unyanyapaa, na kulaumiwa kama wao ndio chanzo cha maambukizi,” amesema mkuu huyo wa WHO.

Wanawake ni jawabu na si tatizo la Chagas

Anaweka bayana kuwa “wanawake si tatizo, bali wao ndio kitovu cha jawabu la tatizo hilo.”

Kwa mantiki hiyo “WHO inatoa wito kwa kila nchi kuongeza mipango ya kufanyia uchunguzi wanawake na wasichana wenye umri wa kujifungua mtoto, kupatia tiba kila mmoja wao anayehitaji na kumfanyia uchunguzi kila mtoto mchanga anayezaliwa au aliyepata maambukizi kutoka kwa mama,” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa “kwa pamoja tunaweza kuvunja mzunguko wa maambukizi, kulinda kizazi kijacho na kufanya ugonjwa wa Chagas kubakia historia.”

🌿 Ugonjwa wa Chagas ni nini? -WHO

Ugonjwa wa Chagas ni maradhi yanayoweza kuhatarisha maisha, yanayosababishwa na vijidudu au parasite aina ya Trypanosoma cruzi. Kwa mujibu wa WHO kwa kawaida, ugonjwa huu hupatikana zaidi katika Ukanda wa Amerika Kusini, lakini kutokana na safari na uhamiaji, visa vya ugonjwa huu vimeripotiwa pia katika maeneo mengine duniani.

🦟 Husambazwa vipi?

Ugonjwa huu huenea zaidi kupitia kung’atwa na mdudu anayejulikana kama “kissing bug” kwa sababu hupenda kung’ata sehemu za uso kama vile mdomo au macho wakati mtu amelala.
Pia unaweza kuambukizwa kupitia:

  • Kuchangia damu
  • Upandikizaji wa viungo vya mwili
  • Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito
  • Kula chakula kilicho na vimelea

🩺 Dalili zake ni zipi?

Ugonjwa wa Chagas una hatua mbili:

  1. Hatua ya awali: wiki au miezi michache baada ya maambukizi
    • Mara nyingi hakuna dalili au dalili huwa hafifu
    • Wengine hupata homa, uchovu, macho kuvimba, maumivu ya mwili, upele
    • Watu wengi huwa hawajui kama wameambukizwa
  2. Hatua ya muda mrefu: miaka baadaye endapo haitatibiwa
    • Huathiri moyo, mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, na mfumo wa neva
    • Takribani asilimia 30 ya wagonjwa hupata matatizo ya moyo, na asilimia 10 matatizo ya tumbo au neva

💊 Je, unatibika?

Ndiyo- ukiugundua mapema, ugonjwa huu unatibika kwa kutumia dawa za kuua vimelea kama benznidazole au nifurtimox.
Katika hatua ya muda mrefu, matibabu husaidia kudhibiti dalili na kupunguza kasi ya madhara makubwa.

📌 Kwa nini ugonjwa huu ni hatari?

Ingawa unaathiri mamilioni ya watu hasa katika maeneo ya vijijini na maskini mara nyingi hupuuzwa kwa sababu dalili zake huwa za taratibu na zinaweza kujificha kwa miaka mingi.
Ndiyo maana mashirika kama WHO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF yanafanya kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa huu kila mwaka Aprili 14 katika Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Chagas.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *