
Taarifa ya WFP iliyotolewa leo huko Darfur Kaskazini, Sudan, imesema watu wa nchi hiyo bado wameachwa wakikabiliana na mapigano makali na mateso yaliyosambaa.
“Jamii ya kimataifa imeshindwa kuzuia na kumaliza mzozo huu na kushindwa kuwalinda watu wa Sudan dhidi ya ukatili,” amesema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau, ambaye ndio kwanza amerejea kutoka Darfur.
Ameongeza kuwa“Watu niliokutana nao kwenye kambi wamepitia maisha ya jehanamu, wamekimbia nyumba zao na kuacha kila kitu nyuma na sasa wanaishi kwenye mazingira ya kusikitisha sana. Wanastahili maisha bora zaidi, na ni lazima tuhakikishe kuwa hawataangushwa tena kwa kuwapa msaada wa msingi wanaouhitaji.”
Zaidi ya watu milioni 19 bado wanakabiliwa na njaa kali nchini Sudan, na baadhi ya maeneo yanaendelea kukabiliwa na tishio la njaa kubwa huku ghasia, watu kuhama makazi yao, na kuporomoka kwa uchumi vikiendelea.
Kwa mujibu wa WFP jamii zimetengwa na upatikanaji wa chakula, masoko, na misaada, huku watoto wakilazimika kukosa elimu kwa miaka mitatu, jambo linaloweka mustakabali wao hatarini. Sudan inasalia kuwa mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, huku karibu theluthi mbili ya idadi ya watu sasa wakiwa na uhitaji wa haraka wa msaada ili kuishi.
Athari za mzozo wa Mashariki ya kati kwa sudan
Hali ya njaa nchini Sudan sasa iko hatarini kuchochewa zaidi na kuongezeka kwa mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati, ambapo machafuko kwenye Bahari ya Shamu au Red Sea yanachelewesha uingizaji wa bidhaa muhimu na kupandisha gharama za chakula, mafuta na mbolea.
Bei ya mafuta nchini Sudan imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 24, hali inayopandisha bei ya chakula na kuwaacha mamilioni ya watu washindwe kumudu mahitaji ya msingi.
Matatizo haya pia yanaathiri moja kwa moja shughuli za kibinadamu kupitia ucheleweshaji wa shehena na gharama kubwa za usafiri, jambo linaloweza kuzitumbukiza familia nyingi zaidi kwenye uhaba wa chakula, ambapo Carl Skau ameonya.
“Wanawake niliozungumza nao kote nchini Sudan wameniambia kuwa hawana chakula cha kutosha cha kuwalisha watoto wao na hawana uwezo wa kupata huduma muhimu za msingi. WFP na jumuiya ya kibinadamu tuna uzoefu na uwezo wa kuongeza msaada wetu, lakini ili tufanye hivyo, tunahitaji msaada wa kibinadamu uruhusiwe kupita kwa uhuru, usalama, na kwa kiwango kikubwa na tunahitaji ufadhili zaidi.”
Ni zipi juhudi za WFP?
WFP inatoa kipaumbele kikubwa kwenye maeneo yenye njaa kubwa na yale yaliyo magumu kufikika, ikifikia watu milioni 3.5 kila mwezi kwa msaada wa dharura wa chakula, fedha taslimu, na lishe. Theluthi mbili ya wale wanaosaidiwa na WFP wako jimbo la Darfur na Kordofan, ambako njaa imethibitishwa na mapigano ni makali zaidi, huku watoto zaidi ya milioni mbili walio chini ya miaka mitano na zaidi ya wanawake 500,000 wajawazito na wanaonyonyesha wakifaidika na lishe mwaka 2025.
Aidha, shirika hilo linaimarisha mifumo ya chakula ya ndani ambapo msimu uliopita, wakulima walioungwa mkono na WFP walizalisha karibu sehemu moja ya tano ya ngano ya nchi hiyo, jambo linaloimarisha uchumi wa ndani na kupunguza uhaba wa chakula.
Msaada wa chakula wa WFP umepungua kwa asilimia 14 tangu Januari ikilinganishwa na mwaka jana kutokana na uhaba wa rasilimali. Shirika hilo linahitaji kwa haraka zaidi ya dola za Kimarekani milioni 600 ili kuendeleza operesheni za kuokoa maisha nchini Sudan kwa miezi sita ijayo.