Jumla ya watoto 89 wameuawa au kujeruhiwa ndani ya mwezi Machi 2026 pekee.  Hilo ni ongezeko la asilimia 65 ikilinganishwa na mwezi Februari, jambo linalodhihirisha jinsi mashambulizi hayo yanavyozidi kuangamiza familia na jamii hata maeneo yaliyo mbali na mstari wa mbele wa vita.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, iliyotolewa leo huko mji mkuu wa Ukraine, Kyiv inaeleza kuwa hali hii ya hatari imejitokeza wazi kufuatia mashambulizi makali yaliyotokea usiku wa kuamkia leo Aprili 16, 2026 katika miji ya Dnipro, Kharkiv, Kyiv, na Odesa.

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 ameuawa akiwa mji mkuu, Kyiv, mahali ambapo palipaswa kuwa kimbilio na salama kwake, huku watoto wengine wengi wakiripotiwa kujeruhiwa kote nchini. Katika kipindi cha kwanza cha mwaka huu wa 2026, idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa imeongezeka kwa asilimia 49 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, hali inayoashiria kuwa usalama wa watoto unazidi kupotea.

Hakuna mtoto aliye salama

Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine, Anne-Claire Dufay, amesisitiza, “hakuna mtoto aliye salama hapa nchini, wote wanaishi chini ya tishio la mashambulizi kila wakati popote walipo.”

Tangu kuanza kwa vita hivi mnamo Februari 2022, jumla ya watoto 3,452 wamethibitishwa kuuawa au kujeruhiwa na Umoja wa Mataifa, ingawa idadi halisi inahofiwa kuwa kubwa zaidi.

“Mashambulizi haya yameacha makovu makubwa ya kihisia kwa wapendwa wao na jamii nzima. Hakuna familia inayostahili kupata maumivu haya makali,” ameeleza Anne-Claire.

Mbali na vifo, vita vimezifanya familia na watoto kukimbia makazi yao mara kwa mara, ambapo utafiti wa UNICEF unaonesha kijana mmoja kati ya watatu wenye umri wa miaka 15 hadi 19 amehama makazi zaidi ya mara mbili. Aidha, miundombinu muhimu kama shule, vituo vya afya, na mifumo ya maji na umeme imekuwa ikilengwa na kuharibiwa, jambo linalokwamisha maendeleo na ustawi wa watoto. Hali hii imesababisha watoto wengi kukosa haki zao za msingi za elimu na huduma za kijamii kwa sababu ya hofu ya usalama wao.

Sheria za kimataifa ziheshimiwe

Ili kukabiliana na janga hili, UNICEF na washirika wake wameendelea kutoa msaada wa dharura ikiwemo; maji safi kwa watu milioni 1.8 na msaada wa kisaikolojia kwa watoto na walezi 116,000. Shirika hilo limetoa wito wa dharura wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za binadamu na kukomeshwa kwa ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto. Ukraine inahitaji amani ya kudumu itakayolinda haki za watoto na kukuza ustawi wao, huku ikisisitizwa kuwa watoto lazima walindwe dhidi ya mashambulizi wakati wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *