Dar es Salaam. Wakati mrembo wa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya urembo duniani akitarajiwa kutangazwa Aprili 19, 2026 kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki imeibuka sintofahamu kwa baadhi ya wadau.

Katika sintofahamu hiyo wapo wanaohoji, inakuwaje mrembo wa kuiwakilisha Tanzania duniani, hatokei kwenye shindano la Miss Tanzania kama ilivyozoeleka. Badala yake anatokea kwenye shindano jipya la Mustafa Hassanali liitwalo Miss World Tanzania.

Hayo yameleta mjadala mkali baada ya Aprili 14, 2026, Mkurugenzi wa kampuni ya The Look, Basila Mwanukuzi kukabidhi umiliki wa uandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania kwa kampuni ya Lamata Village Entertainment inayomilikiwa na mwongoza filamu nchini Leah Mwendamseke ‘Lamata’.

Makabidhiano hayo yalifanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali.

Kushoto Mkurugenzi wa Lamata Village Leah Mwendamseke ‘Lamata’  akikabidhiwa kijiti cha kuendesha mashindano ya Miss Tanzania na Mkurugenzi wa kampuni ya The Look, Basila Mwanukuzi

Ikumbukwe Basila alipokea shindano hilo kutoka kwa marehemu, Hashim Lundenga aliyekuwa analisimamia tangu mwaka 1994 hadi 2018 ambaye aliwatoa warembo wengi akiwamo Nancy Sumari alifika hatua ya kuwa Miss Afrika katika Shindano la Miss World mwaka 2005.

“Tulibeba slogani ya urembo ni heshima na kweli tumeheshimisha Tanzania. Lakini ni bado jukwaa la kutoa warembo wengine wataofanya mambo makubwa zaidi. Na leo historia inaenda kuwekwa nchini Tanzania. Hili jukumu nililichukua muda mrefu.

“Na sio tu biashara nimewekeza natakiwa nijue namwachia nani, walijitokeza hadi Waturuki wenye fedha zao wanataka brand ya Miss Tanzania. Lakini siwezi kufanya hivyo kwa sababu nina deni.

“Ilinichukua muda mimi namatumaini makubwa sana na mwanzo wa siku hii ya leo, Lamata historia yake inafahamika mimi pia sina shaka tunatakiwa kumsapoti na kusapoti mabinti zetu,” alisema Mwanukuzi wakati wa kukabidhi kijiti hicho.

Hata hivyo sintofahamu haikuishia kwenye mrembo atayepelekwa Miss World itayofanyika Vietnam Agosti 9 hadi Septemba 5, 2026. Badala yale wapo waliohoji Basila ameweza vipi kukabidhi leseni kwa mtu mwingine wakati alikuwa amefungiwa kuliendesha shindano hilo.

Pia watu wanajiuliza itakuwaje kwa Lamata kumsaka Miss Tanzania atakayekwenda kuwakilisha nchi kwenye Miss World wakati kuna mtu mwingine tayari anafanya shughuli hiyo kwa sasa.

Ishu iko hivi…

Ikumbukwe moja ya sababu ya Basila kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ilikuwa  kushindwa kumpeleka mshindi wa shindano hilo mwaka  2024/2025 kwenye shindano la Miss World.

Hashim Lundenga aliyekuwa anasimamia mashindano ya Miss Tanzania tangu mwaka 1994 hadi 2018

Licha ya Basata kumfungia, Basila alikata rufaa na kwenda Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, kukata rufaa ambayo hadi leo hakuna majibu ya nini kiliamuliwa mpaka juzi watu walivyoona akikabidhi shindano hilo kwa mtu mwingine.

Mwananchi imezitafuta mamlaka zinazosimamia sanaa nchini ikiwamo Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia  Mkurugenzi wa Sanaa na Utamaduni, Dk Emmanuel Ishengoma, kutaka kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Katika maelezo yake Dk Ishengoma amesema sakata lililokuwa linahusu kufungiwa kuendesha shindano la Miss Tanzania lilikuwa linamuhusu mtu na sio ‘brand’ hivyo kukabidhiwa kwa mtu mwingine haina shida.

“Miss Tanzania ni brand’ na sio mtu, ndio maana unaona linaweza kutoka kwa mtu mmoja akasimamia mtu mwingine.

“Katika lile sakata la kusimamishwa kuendesha shindano lilikuwa linamuhusu mtu binafsi na sio brand ya Miss Tanzania. Hivyo kama kuna mtu kauza brand yake na kufuata masharti na vigezo vyote vilivyowekwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kwetu hiyo haina shida,”amesema Dk Ishengoma.

Hata hivyo Mwananchi ilitaka kujua inakuwaje kuna mtu anaandaa shindano la kumsaka mrembo atakayewakilisha Tanzania Miss World halafu tena inaonekana kuna mtu anakabidhiwa shindano la Miss Tanzania.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Edward Buganga, amesema mashindano ya warembo nchini yapo mengi ila kuna leseni maalum inayotolewa ya kupeleka mrembo kwenye shindano la kumsaka mlimbwende wa dunia ‘Miss World’.

Buganga amesema leseni hiyo kwa sasa  amepewa mbunifu wa mavazi, Mustapha Hasanal na tayari yupo katika michakato hiyo ambapo fainali zake ni siku ya Jumamosi.

“Kwa kuwa Hasanali ndio anatafuta Miss World Tanzania kwa sasa, mrembo wake atakayepatikana ndio atawakilisha Tanzania kwenye Miss World,” amesema Katibu huyo.

Kuhusu ishu ya Basila na Lamata kuuziana haki ya Miss Tanzania, amesema ni makubaliano tu wamefikiana kuuziana kwa kufuata taratibu zote ambapo kwenye mkataba wao tusingependa sana kuingilia kwa kuwa hayo ni mambo ya kisheria zaidi.

Mwasisi wa onyesho Swahili Fashion Mustafa Hassanali, ambaye kwa sasa anaendesha mashindano ya kumsaka Miss World Tanzania 

“Sisi tunachoangalia hapa zaidi ni mtu anayekuja kuomba kibali cha shindano hilo  tunaangalia tu nyaraka za aliyekabidhiwa kuliendesha kama zinakidhi vigezo na masharti yetu ya kuliendesha.

Hata hivyo katika hili Basata wanasema hata kama Lamata Village itaandaa shindano la kumpata Miss Tanzania kwa mwaka huu, hataweza kumpeleka mshindi kwenye shindano la Misa World kwa kuwa tayari kuna aliyepewa leseni ya kufanya hivyo.

Kuhusu Basila sakata lilikuwa ni kutopeleka Miss Tanzania wake Miss World na ndio maana waandaji wa shindano hilo la dunia wamempa leseni mtu mwingine.

Sio lazima Miss Tanzania aende Miss World

Wakati watanzania walio wengi wakidhani Miss Tanzania ndio lazima aende Miss World, Basata imefafanua hili kuwa sio kweli.

Badala yake, Bugaga amesema anaweza kutoka katika shindano lolote la urembo kikubwa awe amekubaliwa kupata leseni waandaaji wa Miss World.

Hata hivyo kwa Tanzania anasema ilijengeka hivyo kwa kuwa shindano kubwa la urembo lilikuwa Miss Tanzania licha kuwapo kwa mashindano mengine kama Miss Utalii, Miss Grand, Miss Universe na mengine mengi.

Kwa mujibu wa katibu huyo, katika nchi nyingine kati ya mashindano tajwa hapo unakuta mojawapo mshindi wake ndio wanampeleka Miss World.

Aidha akitoa maoni yake aliyewahi kuwa mwaandaji wa Miss Kinondoni, Somoe Ng’itu, amesema Basila hajakabidhi shindano kwa tasnia ya filamu bali kwa kampuni ya  ‘Lamata Village’ ambayo ipo chini ya Lamata.

Hivyo anachotakiwa kufanya Lamata ni kutofautisha  sanaa ya filamu au maigizo na sanaa ya  urembo kwa kuwa ni vitu viwili tofauti.

“Kwa hiyo anachotakiwa ni aende na misingi ya kazi ambayo ameipokea, ikiwamo kujua sifa za warembo, mashindano yana maadili gani na kujua vitu gani vinatakiwa katika shindano hilo na hapo ndipo atafanikiwa,” amesema.

Hata hivyo Somoe amesema kwa kuwa Lamata  amekuwa katika tasnia ya sanaa muda mrefu, anawafahamu wadau ambao wanaweza kumsapoti na hivyo kufanikiwa upande mmoja kunaweza kumsaidia kama tiketi  kufanikiwa katika jambo hilo la shindano.

Pia ameshauri kwa kuwa shindano tangu lilipotoka chini ya usimamizi wa Hashim Rundenga, lilishuka kama timu iliyoshuka daraja. Ni vema kupambana kulipandisha shindano hilo kubwa la urembo nchini na kuleta ushindani na kulirudishia uhai wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *