DODOMA: serikali imelenga kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uanzishwaji na uendeshaji wa biashara kwa kufanya mapitio ya sheria na kanuni ambazo sio rafiki kwa biashara, kupunguza au kufuta tozo na ada zenye kero kwa wafanyabiashara, pamoja na kuondoa mwingiliano wa majukumu miongoni mwa taasisi za udhibiti.

‎Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

‎Prof. Mkumbo amesema ofisi yake imefanikiwa kufanya mapitio ya jumla ya sheria 28 zilizokuwa zikikwamisha mazingira ya biashara, sambamba na hilo, jumla ya tozo na ada 245 zimefutwa au kupunguzwa ili kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara.

‎Ametaja baadhi ya maboresho yaliyofanyika kuwa ni pamoja na kupunguza ushuru wa huduma (service levy) kutoka asilimia 0.3 hadi 0.25 ya pato ghafi kupitia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, kupunguza ushuru wa hoteli kutoka asilimia 10 hadi 2, pamoja na kufuta ada za upakiaji na upakuaji katika baadhi ya mamlaka za serikali za mitaa.

‎”Vilevile, Serikali imerejesha kanuni nafuu za usimamizi wa mazingira za mwaka 2021 na kuimarisha udhibiti wa utozwaji wa ada na tozo kupitia marekebisho ya Sheria ya Bajeti na Sheria ya Fedha za Umma.” Amefafanua Prof. Kitila.

‎‎Aidha, Serikali imejikita katika kuanzisha na kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma ili kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha zaidi kufanya biashara nchini.

‎Lengo la maboresho hayo ni kujenga mazingira rafiki, yanayotabirika na yenye ushindani kwa wawekezaji wa ndani na nje, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira.

‎‎Kwa mujibu wa Waziri huyo, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kwa kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuongeza motisha kwa wawekezaji, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *