Dar es Salaam. Chama  Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeeleza kuwa kina imani na tume ya uchunguzi inayoongozwa naJaji mstaafu, Mohamed Chande kuhusu matukio ya Oktoba 29, kikisema wajumbe wake wana weledi na uadilifu wa hali ya juu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mrema, amesema muundo wa tume hiyo unatoa matumaini ya kupatikana kwa majibu sahihi na ya haki.

Alisema tume hiyo imeundwa na Rais kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kuelewa ukweli wa matukio yaliyotokea, huku akisisitiza kuwa ina watu wenye sifa na uzoefu unaotambulika ndani na nje ya nchi.

“Kwa kuangalia wajumbe wake, akiwemo Jaji Chande, tunaona wazi kuwa ni watu wenye historia na wasifu wa kimataifa. Hata tume aliyoiendesha mwaka 2023 ilifanya kazi nzuri, na sisi wa upinzani tulikubaliana na matokeo yake,” alisema Mrema.

Alieleza kuwa tume hiyo ni fursa muhimu kwa taifa kupata ukweli na kuwajibisha wahusika, hatua itakayosaidia kujenga mshikamano wa kitaifa.

“Hii ni nafasi ya nchi kuelewa kilichotokea na kuchukua hatua stahiki ili tusonge mbele kwa pamoja kama taifa,” aliongeza.

Aidha, alisema tume hiyo imeongezewa muda wa siku 21 ili kukamilisha kazi yake, na inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ifikapo tarehe 24 mwezi huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *