Marekani. Mkali wa Pop na RnB kutokea Canada, Justin Bieber, (32), anaripotiwa kupokea malipo ya Dola 10 milioni, wastani wa Sh25 bilioni, kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha la Coachella 2026 ambalo limefanyika hivi karibuni huko Marekani.

Malipo hayo yanamfanya kuwa mwanamuziki aliyelipwa fedha nyingi zaidi katika historia ya tamasha hilo akiwa amewapiku mastaa kama Beyonce, Lady Gaga, The Weeknd na Ariana Grande, ambao kila mmoja alilipwa Dola8 milioni.

Hata hivyo, mbali na fedha hizo na heshima kubwa aliyopata kutoka kwa mashabiki waliohudhuria, huu ni mwanzo wa safari yake mpya baada ya kupitia changamoto za kibiashara zilizomuacha na madeni.

JUSTI 01

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rolling Stone mnamo Septemba 2025, chanzo kimoja kililiambia Jarida hilo ni hatua ya kihistoria kwa mtumbuizaji mkuu wa tamasha hilo kulipwa vizuri namna hiyo.

Bieber aliyetoka na albamu yake, My World 2.0 (2010) iliyoshika namba moja Billboard 200, alipata dili hilo moja kwa moja kutoka kwa waandaaji wa Coachella ambao ni kampuni ya Goldenvoice.

“Hadi kuwa msanii mkuu wa Coachella na mafanikio ya albamu yake mpya, ni wazi huu ni mwanzo wa enzi mpya ya kusisimua kwa Justin Bieber – enzi ambayo yeye ndiye dereva wake,” chanzo hilo kilieleza.

JUSTI 06

Ikumbukwe Bieber amepata dili hilo bila kupitia kwa meneja kwa sababu hajaajiri meneja tangu alipoachana na Scooter Braun mwaka 2023 baada ya ushirikiano wa kikazi kwa takribani miaka 15.

Mnamo Julai 2025, Bieber alimaliza mgogoro wa kifedha na Braun kwa kuilipa kampuni yake, Hybe zaidi ya Dola8.8 milioni.

Braun alikuwa amemkopesha Bieber fedha hizo mnamo 2020 ili kulipia sehemu ya mkopo wa Dola 40 milioni uliotolewa na Anschutz Entertainment Group (AEG) kufadhili ziara yake ambayo baadaye iliahirishwa.

Miaka hivi karibuni ilielezwa Bieber alikuwa akikabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na kufanya maamuzi mabaya yaliyoathiri uhusiano wake na watu, fedha na biashara.

JUSTI 02
JUSTI 06

Mmoja wa watu waliokuwepo katika menejimenti yake aliuambia mtandao wa The Hollywood Reporter kuwa msanii huyo amepoteza mwelekeo wa kibiashara.

“Tunamuona akipotea hivi hivi… ni kama kutazama mfano halisi wa mtu asiyeishi kusudi lake,” chanzo hicho kilisema na kuongeza.

“Amepotea, hakuna anayemlinda kwa sababu hakuna mtu anayetaka kuwa karibani naye. Unapomwambia hili hapana, anakufukuza,” chanzo hicho kilieleza. 

JUSTI 05

Chanzo hiki ndicho kiiibuka madai ya Bieber kudaiwa mamilioni ya dola baada ya kugharisha ziara yake (Justice Tour) ya kimuziki na alitarajiwa kufanya matamasha kadhaa lakini sasa ameshamalizana na hayo.

Kwa sasa staa huyo wa kibao, Never Say Never (2011), yupo tayari kwa mwanzo mpya na mashabiki wanategemea mengi baada ya show yake ya Coachella ambayo pia imeongeza mauzo ya nyimbo zake mtandaoni.

Kutumbuiza Coachella kumekuja kufuatia mapokezi mazuri ya albamu yake ya saba, Swag (2025) akivunja ukimya wa muda mrefu tangu alipotoa ya albamu ya Justice (2021). Hata hivyo, Septemba 5, alitoa albamu nyingine kubwa yenye nyimbo 44, Swag II (2025).

JUSTI 03

Albamu hiyo ameiandika kama sehemu ya shukrani kwa mkewe Hailey ambaye walikutana kwa mara ya kwanza Novemba 2009 katika kipidi cha Today Show, kisha kuja kufunga ndoa Septemba 2018 huko New York.

Baadhi ya nyimbo ambazo zimemzungumzia moja kwa moja Hailey, ni ‘I Do’, ‘I Think You’re Special’ na ‘Mother in You’ ambao pia umekwenda kwa mtoto wao wa mwaka mmoja, Jack Blues.

Katika mahojiano na Podcast ya Therapuss mnamo Februari, Hailey alizungumzia muziki wa mume wake na kutaja albamu anazozipenda zaidi kutoka kwake.

Albamu ya kwanza ni Journals (2013), na ya pili ni Purpose (2015) yenye nyimbo kali kama What Do You Mean?, Sorry na Love Yourself.

JUSTI 04

Kuhusu albamu mpya ya Bieber, Swag (2025), ambayo ilifikia nafasi ya pili kwenye chati ya Billboard 200, Hailey alisema. “Ni albamu nzuri sana kuisikiliza kuanzia mwanzo hadi mwisho,”.

“Ni wazi labda nina upendeleo kidogo, lakini nadhani ishara ya albamu nzuri ni ile ambayo baada ya muda unarudi kuisikiliza tena na tena, na mimi bado naendelea kuirudia mara kwa mara,” aliongeza.

Mbali na kuwa mke na mama mtoto wao, Hailey anagusa maisha ya Bieber kiuchumi kupitia biashara zake za urembo na mitindo. Mei 2025, kupitia chapa yake, rhode ambayo yeye ni Mwanzilishi na Mkuu wa Ubunifu, waliingia makubaliano ya kibiashara na chapa ya vipozi ya e.l.f. cosmetics.

Makubaliano hayo yenye thamani ya Dola1 bilioni, wastani wa Sh2.6 trilioni, ni kitu kilichomfurahisha sana Bieber, mkali wa kibao, Sorry (2015).

“Nilipozindua Rhode mnamo 2022, siku zote nilikuwa na ndoto kubwa kwa kampuni hii, na jambo la muhimu zaidi kwangu ni kuendelea kuisogeza Rhode karibu zaidi na ulimwenguni,” alisema Hailey.

Miongoni mwa mastaa waliompongeza Hailey, ni pamoja na Kylie Jenner na Kim Kardashian ambaye utajiri wake wa Dola1.7 bilioni kwa sehemu kubwa unatokana na mikataba minono anayosaini kupitia chapa zake za mavazi na vipodozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *