Mtwara. Wajumbe wa Kamati ya Uchumi na Uwekezaji ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeridhishwa na maendeleo ya miradi ya gesi asilia inayotekelezwa mkoani Mtwara, ikieleza kuwa hatua zilizofikiwa zinaashiria mafanikio makubwa katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za taifa.

Akizungumza leo Aprili 17, 2026 wakati wa ziara ya mafunzo na ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Makame Sufuani, amesema uzoefu walioupata ni wa thamani kubwa kwa Zanzibar katika jitihada za kuendeleza sekta ya nishati.

Amesema usimamizi mzuri wa miradi ya gesi umechangia kuimarika kwa huduma za umeme na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali, hali inayochochea ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.

“Tumeridhishwa na kazi kubwa inayofanyika hapa Mtwara. Huu ni mfano mzuri wa namna rasilimali za taifa zinavyoweza kusimamiwa kwa tija na kuwanufaisha wananchi,” alisema Sufiani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Mboja Mshenga, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza hatua za awali za ukusanyaji wa takwimu na tafiti ili kubaini uwepo wa gesi asilia na mafuta visiwani humo.

Amesema hatua hiyo italeta mwanga katika maandalizi ya kuanza shughuli za uchimbaji, pamoja na kufungua fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tumeanza hatua za msingi za utafiti ili kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa Zanzibar na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Mshenga.

Awali, akipokea ugeni huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kutumia vyema ziara hiyo kujifunza kwa kina na kuwa mabalozi wa kuitangaza Mtwara pamoja na fursa zake za uwekezaji.

“Mtwara imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo gesi asilia, hivyo ni muhimu kuzitangaza ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuchochea maendeleo ya uchumi,” alisema Msengi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Khalfan Khalfan, amesema ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote za Muungano.

Amesema ushirikiano huo unatoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kiufundi na kitaalamu katika utafutaji, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.

Wajumbe hao, wamesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa na wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata ili kuimarisha sekta ya nishati Zanzibar na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Ziara hiyo imelenga kuwajengea wajumbe wa Kamati ya Uchumi na Uwekezaji uelewa wa kina kupitia uzoefu wa vitendo katika usimamizi wa rasilimali za gesi asilia, kubadilishana maarifa ya kitaalamu na kujifunza mifumo bora ya uendeshaji wa miradi ya nishati. Maarifa hayo yanatarajiwa kutumika kuimarisha sekta ya nishati Zanzibar, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na hatimaye kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi wa visiwa hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *