Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatumai Hezbollah watajiendesha vizuri katika kipindi hicho cha siku kumi alichokiita kipindi muhimu kwao.

Chanzo cha picha, Reuters

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon kwa siku kumi zijazo yameanza kutekelezwa.

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Marekani yanatarajiwa kurahisisha uwezekano wa mazungumzo ya kuvimaliza vita vya Iran.

Kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah limedokeza litayaheshimu makubaliano hayo.

Saa chache tu baada ya kutangazwa kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yameanza kutekelezwa kati ya Lebanon na Israel, Jeshi la Lebanon limeripoti kuwa Israel imeyakiuka kwa kushambulia vijiji kadhaa vya kusini mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo limewatahadharisha wakaazi wa Kusini mwa Lebanon kutorejea makwao kwasababu hali bado ni tete.

Israel imesisitiza kuwa Majeshi yake yatasalia katika maeneo inayoyadhibiti.

Iran imesema imepokea vyema makubaliano hayo ya kusitisha vita lakini imetaka majeshi ya Israel kuondoka kabisa Lebanon.

Zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mashambulizi hayo na zaidi ya watu milioni moja na laki mbili wameachwa bila ya makazi.

Aidha Bwana Netanyahu amesema hajakubaliana na matakwa ya Hezbollah ya kuyaondoa majeshi yake kusini mwa Lebanon na kusisitiza kuwa kutasalia kile alichokitaja eneo salama mpakani na Lebanon na hadi mpaka wa Syria.

Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Steffane Dujarric amesema wamefurahishwa na hatua zilizochukuliwa na Israel na Lebanon kusitisha mapigano.

Iwapo makubaliano hayo yatadumu basi huenda ikasafisha njia ya kufikiwa makubaliano ya amani kati ya Israel, Marekani na Iran na itakuwa ushindi mkubwa kwa utawala wa Trump ambao umekuwa ukipata tabu kukabiliana vilivyo na Iran hususan kuishinikiza kufungua Mlango Bahari wa Hormuz na kuachana na mpango wake wa Kinyuklia.

Soma zaidi:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *