Mtama. Wavuvi wanaovua maeneo ya Sudi ,Shuka na Mmongomongo  wametakiwa kukata leseni ya uvuvi ili kutambulika na serikali na kuweza kupata mikopo hasa ya boti za uvuvi kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi kupitia   Halmshauri yao .

Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani Robo ya tatu (Januari hadi Marchi) leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mtama Anderson Msumba amesema kuwa wavuvi wote wanaovua katika Halmshauri ya Mtama wanatakiwa kukata leseni ili waweze kutambulika na Serikali.

Amesema pia wanapotambulika wananafasi kubwa ya kupata mikopo kupitia Halmshauri pamoja na wadau mbalimbali kuweza kuwakopesha boti kwa wavuvi pamoja na vifaa vingine ambavyo vinahusu uvuvi.

Msumba ameendelea kusema kuwa uvuvi usiotambulika unachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa mapato kwani mvuvi anatakiwa akishatoka kuvua, auze samaki kwenye eneo lililotengwa na kutoa ushuru kwa Halmshauri.

“Ninawaomba wavuvi wote wanaovua maeneo niliyoyataja wajitahidi kukata leseni kwani sasahivi mvuvi akishatoka kuvua anakwenda kuuza samaki zake nje ya eneo husika kwakuwa hakuna sehemu maalumu ya kuuzia samaki napia tunapoteza mapato kwani hakuna ushuru tunaoukusanya.”amesema Msumba.

Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mtama Yusuph Tipu (Wapili kutoka kulia )akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani robo ya tatu(Januari _Marchi). Picha na Bahati Mwatesa

Aidha Ofisa Uvuvi kutoka Halmshauri ya Mtama Hussein Mkama, amesema kuwa kwenye Halmshauri ya Mtama kuna kata tatu ambazo zinajishughulisha na uvuvi ikiwemo kata ya Navanga,kata ya Sudi pamoja na kata ya Nachunyu,ambapo amesema kuwa wavuvi wapatao 570 wanavua katika Halmshauri hiyo lakini wavuvi 200  ndiyo waliokata leseni na kutambuliwa.

Amesema kuwa wavuvi wengi wamekuwa wakiuza samaki nje ya eneo lao na kushindwa kukusanya mapato ya Halmshauri.

“Wavuvi  200 ndiyo wamejisajili na wanatambulika niwaombe  wale ambao bado hawajajisajili waje wajisajili ili tuwatambue kwani ukitambulika  nirahisi kupata  mikopo ambayo inayotolewa na Wizara ya Mifugi na Uvuvi  kupitia Halmashauri.”mesema Mkama.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mtama Yusuph Tipu amewataka madiwani wa Halmshauri hiyo kushirikiana na viongozi wa Halmshauri katika kutatua changamoto za wananchi kwenye maeneo yao.

“Tuendelee kushirikiana na viongozi wetu katika kutatua changamoto za wananchi,jambo kama unaweza kulijibu wewe diwani lijibu ,tusisubiri hadi vikao,tukifanya kazi kwa ushirikiano tutakuwa tumeijenga Halmshauri yetu na kuleta maendeleo.”amesema Tipu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *