Kulingana na uchambuzi wa hivi karibuni ya tathimini ya viwango vya uhakika wa chakula IPC, takriban watu milioni 5.8 sawa na asilimia 52 ya idadi ya watu nchini humo wanakabiliwa na viwango vya mgogoro wa chakula au hali mbaya zaidi viwango vya IPC daraja la 3 au zaidi kati ya Machi na Juni 2026.

Kati yao, zaidi ya watu milioni 1.8 wanakabiliwa na hali ya dharura ya njaa  viwango vya IPC Daraja la 4, ikimaanisha wanatumia rasilimali zao za mwisho na hawawezi kukidhi hata mahitaji ya msingi ya chakula.

Mafanikio madogo yako hatarini kutokana na gharama

Licha ya hali hiyo mbaya, WFP inasema kulikuwa na maboresho madogo mwaka 2025. Kwa kushirikiana na serikali na wadau wa kibinadamu, shirika hilo lilisaidia watu milioni 2.7 kupitia misaada ya chakula ya dharura, programu za lishe shuleni, na msaada kwa wakulima wadogo.

Hata hivyo, mafanikio hayo yanabaki kuwa dhaifu sana.

“Maboresho haya madogo katika takwimu za uhakika wa chakula hayapaswi kutufanya tupuuze hali halisi,” amesema Wanja Kaaria mkuu wa WFP Haiti. “Kupanda kwa bei ya mafuta na gharama za chakula kunahatarisha kufuta mafanikio haya, na kusukuma familia zilizo hatarini zaidi kuingia katika mgogoro mkubwa zaidi na kuzidisha hali ya kutokuwepo kwa utulivu.”

Ameongeza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta duniani kunakohusishwa kwa sehemu na mivutano ya Mashariki ya Kati kunasababisha ongezeko la gharama za usafirishaji na chakula, na hivyo kuongeza mzigo kwa kaya zilizo tayari katika hali mbaya.

Mwanamke mwenye mavazi mekundu amebeba kitanda cha usafi cha UNICEF kichwani mwake na ndoo ya maji mkononi mwake, akitembea kupitia eneo lililoharibiwa nchini Haiti baada ya Kimbunga Melissa.

© UNICEF/Herold Joseph

Mwanamke nchini Haiti anawasili katika kitua cha usambazaji wa chakula.

Njaa inachochea ukosefu wa utulivu na ukatili

WFP imesisitiza kuwa kukabiliana na njaa si suala la kibinadamu pekee bali pia ni muhimu kwa kurejesha utulivu nchini Haiti, ambako vurugu na makundi yenye silaha vinaendelea kusambaa.

“Kukabiliana na njaa ni muhimu katika kurejesha utulivu nchini Haiti. Hatuwezi kujenga amani wakati familia hazina chakula cha kulisha watoto wao,” amesema Kaaria.
Ameongeza kuwa “Njaa hufungua mlango kwa makundi yenye silaha ambayo hutumia hali hii vibaya, yakivutia watoto kwa chakula na kuwanyanyasa wanawake na wasichana wanaojitahidi kuhudumia familia zao.”

Amesisitiza kuwa msaada wa chakula ni nguzo ya kwanza ya ulinzi kwa watu walio hatarini na huchangia kujenga upya mifumo ya chakula ya ndani pamoja na matumaini ya baadaye.

Miaka ya migogoro imechangiwa na vurugu na majanga ya asili

Kwa karibu muongo mmoja sasa, Haiti imekuwa ikikabiliwa na mgogoro unaozidi kuongezeka wa uhakika wa chakula, unaochangiwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, mdororo wa uchumi, vurugu za magenge yenye silaha, na majanga ya tabianchi.

Hali ilizorota zaidi baada ya athari kimbunga Melissa kilichopiga maeneo ya kusini mwishoni mwa mwaka 2025, na kuongeza changamoto zilizokuwepo tayari.

Vurugu zinazoendelea zimesababisha watu zaidi ya milioni 1.4 kuyahama makazi yao, huku takriban watu 300,000 wakiishi katika makazi ya muda yaliyofurika pomoni na yasiyo na hali bora ya usafi katika mji mkuu, jambo linaloongeza hatari ya magonjwa na mateso zaidi.

Wito wa dharura wa ufadhili kuendeleza operesheni

Ili kuendeleza shughuli zake na kupanua wigo wa msaada, WFP inaomba dola milioni 332 kwa miezi 12 ijayo.

Endapo ufadhili utapatikana, shirika hilo linapanga kuwafikia zaidi ya watu milioni 2.7 kwa msaada wa chakula wa dharura na programu za kujenga mnepo.

WFP imeonya kuwa bila msaada wa haraka na endelevu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, mafanikio yaliyopatikana kwa shida yanaweza kufutika haraka, na kuwaacha mamilioni ya Wahaiti katika hatari kubwa ya njaa, ukosefu wa utulivu na umaskini uliokithiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *