Tukio hilo limetokea leo Jumamosi asubuhi kwa saa za Lebanon wakati timu ya UNIFIL ilikuwa ikiondoa mabaki ya vilipuzi kando ya barabara katika kijiji cha Ghanduriyah, ili kurejesha mawasiliano na vituo vya Umoja wa Mataifa vilivyotengwa.

Msafara huo ulikumbwa na mashambulizi ya risasi ndogo kutoka kwa makundi yasiyo ya kiserikali.

“Kwa masikitiko makubwa, mlinzi mmoja wa amani amefariki dunia kutokana na majeraha yake na wengine watatu wamejeruhiwa, wawili kati yao wakiwa katika hali mbaya,” imesema taarifa ya UNIFIL.

Waliojeruhiwa walipelekwa katika vituo vya afya kwa matibabu. UNIFIL imetoa pole kwa familia na waffanyakazi wenzake mlinzi aliyefariki dunia na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi wote.

UNIFIL yakemea ‘shambulio la makusudi’

Ujumbe huo umekemea vikali tukio hilo ukilitaja kama “shambulio la makusudi dhidi ya walinda amani waliokuwa wakitekeleza majukumu yao,” ukibainisha kuwa kazi ya kuondoa vilipuzi ni muhimu sana katika eneo hilo, hasa kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

UNIFIL imesema “imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku tathmini za awali zikionesha kuwa mashambulizi hayo yalitoka kwa makundi yasiyo ya kiserikali, yanayodaiwa kuwa Hezbollah.”

Ujumbe huo umesisitiza kuwa pande zote zinawajibika chini ya sheria ya kimataifa kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na mali za Umoja wa Mataifa wakati wote.

“Mashambulizi ya makusudi dhidi ya walinda amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na Azimio la Baraza la Usalama namba 1701, na yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita,” imesema taarifa hiyo.

UNIFIL pia imeitaka serikali ya Lebanon kufanya uchunguzi wa haraka na kuwawajibisha waliohusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *