Dar es Salaam.  1994. Siyo leo wala siyo jana. Ni zamani kinoma. Magogoni pale akiishi Ali Hassan Mwinyi (RIP). Eneo la Asha Rose Migiro CCM, akiwepo Horace Kolimba (RIP). Bosi wa Dar es Salaam akiwa Ramadhan Ditopile Mzuzuri (RIP). 

Ndo mwaka ambao mshikaji flan kutoka Kidatu Ifakara Morogoro, Hashimu Lundenga. Akiwa na umri wa miaka 38, alileta mzuka wa Miss Tanzania. Tangu ipigwe stop 1967 na serikali ya Baba la Baba Mwalimu Nyerere. Oyaaa ilikuwa unyamaa.

Theresa Shayo ndiye Miss Tz wa 1967. Na Miss Tanzania baada ya shindano kurejea alikuwa ni Aina Maeda. Mtoto flan, hewani flan, rangi flan, ngozi flan, kama anaishi ndani ya tangazo flan. Ni kwere jombaa alikuwa wa moto siyo kitoto.

1995 ikaja pisi toka Dom Emily Adolf. Hapa nikaelewa kwanini Julius alifanya Dom ndo makao makuu ya nchi. Uliza wale watu waliokuwapo miaka ile, ilikuwa noma sana. Miss Tz aliheshimika kuliko mbunge, hutaki poa tu siyo kesi kivile.

1996 akaibuka Shose mtoto wa Mzee Sinare. Huyu dada aliishi kwenye maombi yangu ‘deile’. Ili nikiwa mkubwa Mungu anibariki nimpate mrembo wa aina yake. Lakini Mungu hugawa mke kwa macho ya rohoni siyo ya nyama kama nilivyotaka.

Saida Kessy, kutoka mitaa ile ya Dogo Janjaro, Sakina, Kijenge Juu na Chini, Unga Limited hadi Ngeranaro. Akawa Miss Tz 1997, hii ilikuwa almasi nyingine katika ardhi ya Benjamin Wiliam Mkapa. Ni nyakati za utandawazi kushika hatamu.

Nchi nzima ilizizima, mali kutoka Arachuga ilifunika pisi za Upanga hadi Kurasini Shimo la Udongo. Hapa hata zawadi kwa mshindi iliongezeka, kama ubongo wangu una ‘gudi memori’. Saida ni dada yake na Feza. Mtazame Feza ili ujue aina ya mali ninayoongelea. 

1998 hapa ndo penyewe sasa. Basila Mwanukuzi, mtoto mrefu kutoka kitaa cha ‘Kino Kleni’. Ni mfano wa kiumbe kinachomiliki ngozi nyororo na adimu. Akawa Miss Tz wa 5 baada ya kuanza upya 1994. Huu mwaka una kitu flan amazing sana.

Ni mwaka ambao Temeke ilitupa mwanamitindo wa muda wote. Namuongelea Miriam Odemba, alikuwa Miss Temeke wa 1998. Taifa alifeli kisha wenye akili zao wakampeleka kwenye mitindo. Sasa huko ndo aliua mbaya hadi Ufaransa, umiza sana steji.

Balozi Hoyce mtoto wa Temu, kwa mara nyingine akaturudisha Arachugani. Ndiye Miss Tz 1999, na Hoyce anabaki kuwa mmoja wa mamiss maarufu zaidi. Kwa sababu nyakati zake magazeti ya udaku yalishika kasi, deile katika kurasa za mbele. 

Jackline Ntuyabaliwe (K-Lynn) akaibeba Dar es Salaam, baada ya miaka miwili kula za uso. Ndiye Miss Ilala na Miss Tz wa 2000. Alikuja na Milenia Mpya, enzi za Y2K. Baada ya Kaskazini kuikimbiza Dar kwa miaka miwili, utawala ukarejea Daslama mjini.

Happyness Magesse (Millen), akashindilia utawala wa Daslam. 2001 akawa Miss Tz. Happy ndie miss mwenye mafanikio zaidi, ni baada ya kuhamia mitindoni. Na huko kapiga sana pesa, akifanyia michongo yake Marekani kwa muda mrefu.

2002 akaja Angela Damas, naye aliibeba bendera ya Daslama. Ni mmoja wa mamis wakimya sana ambao umaarufu wao ulikuwa mfupi. Kwa sababu hawakuwa na mbwembwe nyingi. Kumbuka nyakati hizi washiriki walikuwa ni viwango. Dar iliiteka Miss Tz.

Hawa wote elimu zao zilikuwa ni za kueleweka. Familia zao pia sio haba, ukitaka kuwafahamu zaidi wafuatilie sasa. Utaona wengi wapo maeneo mtambuka, kama Hoyce tayari, Balozi wa Tanzania Usswis. Ndo ilivyo kwa Mamiss wengineo wa miaka ile.

Hata Silyvia Bahame na mwanya wake, Miss Tz 2003. Alikuwa vizuri kichwani hata kabla ya ushiriki wake. Ukimtafuta hata leo utagundua nyakati zile, siyo tu urembo. Na ubongo wa binti ulizingatiwa sana ili kupata Miss Tanzania sahihi. Dar iliendelea kuteka.

Kuna Faraja Kotta Miss Tz 2004, muite Faraja Nyalandu sasa. Na kuna Nancy Sumari Miss Tz 2005. Huyo Nancy, aliweka rekodi ya Miss World, akiwa namba moja Afrika. Hawa nao walitoka katika familia flan ambazo siyo maadili tu, elimu pia likizingatiwa.

Miss Tz 2006. Daadeki… leo, leo kazi ipo leooooo… Hapa ndipo Hashim Lundenga, baada ya tripu ndefu ya Miss Tz. Akamleta bibie Wema Abraham Isaac Sepetu, kama Miss Tz. Shughuli ilikuwa ni pevu kweli kweli, Wema huyu hakika alileta mapinduzi.

Huu mwaka ndiyo uliozalisha mastaa wengi katika maeneo tofauti. Kuanzia Wema, Jokate, Lissa Jensein, Irene Uwoya, Ant Ezekiel na Marika ‘Dizaina’. Huu ndo mwaka wa Makomborelo. Ni mwaka uliotikisa mpaka hii leo na bado wanakimbiza.

Na baada ya 2006, hakuna Miss Tz iliyokuja kufunika tena. Mpaka pale Lundenga alipoanza kukata ringi la kuendesha mashindano haya. Walikuja kina Richa Adhia, Nasreem na wengineo. Lakini ni wazi zama za Miss Tz zilipotea na wale wa 2006. 

Akachukua Basila Mwanukuzi kuendeshaji Miss Tz. Na yeye pia kamuachia Leah Mwendamseke a.k.a ‘Lamata’. Naamini sasa pele limepata mkunaji, shindano hili limepata akili mpya ya dunia ya sasa. Lamata hawezi kufeli tena kama watangulizi wake.

Kama filamu zilionekana kufeli na leo kina Lamata hawa hawa. Wamegeuza filamu kuwa tasnia kimbilio la mabintizi. Kwanini hii Mis Tz ifeli? Yaani Miss Tz ifeli katika nyakati ambayo warembo nk wengi kuliko idadi ya mimea?

Sitaki kusema mengi. Naamini katika Lamata, kutokana na kile anachokifanya kwenye mchongo wa uigizaji. Umiss ni bidhaa na walaji wengi ni wanawake, na dili lolote linalopenda na wanawake kibiashara ni mzuka sana. Hili limeenda. 
Karibu tena Miss Tanzania.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *